Askofu Fredrick Shoo wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambaye pia ni mkuu Mstaafu wa KKKT amesema uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ni mpango wa Mungu kuithibitishia Dunia kwamba wanawake wanao uwezo wa kuongoza nchi, kuliko hata wanaume.
Dk. Shoo ameyasema hayo Jumapili Oktoba 27, 2024, wakati wa ibada maalumu ya kuaga watumishi mbalimbali wastaafu, wakiwemo maaskofu, makatibu wakuu, watunza fedha na wasaidizi wao, waliowahi kulitumikia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, tangu wakati wa Sinodi, mwanzoni mwa miaka ya 1960, hadi wakati huu wa KKKT, Dayosisi ya Kati.
"Ndugu zangu ni dhambi kubwa, kudharau mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii, kwa maendeleo ya Kanisa, hivi sasa kuna mfumo dume ambao umejengwa kwamba wanawake hawawezi, na mfumo huu haupo tu kwa jamii na kwenye siasa, bali upo hata kanisani kuwa wanawake hawawezi, leo nasimama hapa kuzungumza kwa niaba ya wanawake hawa, tuuone mchango wao, na tuwe wa wazo kwamba wanawake wanaweza," amesisitiza Dk. Shoo.
Hivyo, kutokana na hali hiyo, mtaalamu huyo wa masuala ya imani, hasa dini ya Kikristo, ameitaka jamii na Kanisa kwa ujumla, kuzidi kuwaunga mkono wanawake kwenye uongozi, Ili waweze kusimamia maendeleo yanayokusudiwa na jamii husika, pamoja na Serikali yao.
Watanzania wanapaswa kutafakari maneno ya Warumi 13:1: "Kila mtu na atiye mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imewekwa na Mungu." Kwa mafanikio ya uongozi wake ndani ya muda mfupi, ni dhahiri kuwa Mungu yuko pamoja naye na anamtumia kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Aidha juu ya uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na ule mkuu wa mwakani (2025) Dk. Shoo amewataka Watanzania kijitokeza kushiriki zoezi hilo, na kuwachagua wanawake, pia na wanaume lakini wanyenyekevu, ambao jamii inawaona wana hofu ya Mungu, katika utumishi wao wa kuwaletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment