*Yatambulisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Sekta Isiyo Rasmi
(NISS)
*Sasa mwanachama kufungua madai ya mafao kidijitali ‘online’
*Yaweka kipaumbele cha matumizi ya TEHAMA, zaidi ya asilimia 82% sasa
zinafanyika kutumia mifumo
* Yatoa Tuzo kwa Vyombo vya Habari vinavyotekeleza vyema sheria ya NSSF,
yatambua mchango wa wahariri wastaafu
Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Bw. Masha Mshomba ameanika mafanikio mbalimbali ambayo Mfuko
umeyafanya yenye lengo la kumuondolea kero mwanachama na kumsogezea huduma
huko huko aliko kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Pia ametambulisha Skimu ya
Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS).
Bw. Mshomba ameeleza mafanikio hayo tarehe 1 Oktoba 2024 wakati akifungua
mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioshirikisha wahariri
wa vyombo mbalimbali vya habari Nchini, uliofanyika katika ukumbi wa NSSF
Mafao House Ilala, Dar es Salaam.
Amesema wanaipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo
amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya NSSF hasa katika miaka minne
iliyopita ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na wanachama katika
Mfuko tofauti na kipindi cha nyuma na kupelekea thamani ya Mfuko kufikia
trilioni 8.5 tofauti na trilioni 4.8 wakati alipokuwa anaingia
madarakani.
Bw. Mshomba amesema NSSF inaendelea kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya
TEHAMA na sasa shughuli nyingi za NSSF zinafanyika kupitia mifumo na kuwa
mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25, huduma zote muhimu
zitatolewa kupitia mifumo, aidha alifafanua ya kwamba kwa sasa zaidi ya
asilimia 80 ya shughuli za Mfuko zinafanyika katika Mifumo tofauti na
asilimia 42 ya mwaka 2021/22
“Kupitia mifumo ya TEHAMA, NSSF imeweza kuwafikia kwa ukaribu wanachama na
wadau wake ambapo kwa sasa hawalazimika kufuata huduma ofisini badala yake
wanazipata huko huko waliko na hivyo tumewaondolea adha ya kufuata huduma
umbali mrefu,” amesema Bw. Mshomba.
Aidha, amesema NSSF imezindua mfumo unaomuwezesha mwanachama kufungua madai
ya mafao kwa njia ya mtandao na kuwa lengo ni kumrahisishia mwanachama
kupata huduma karibu zaidi bila ya kufika katika ofisi za NSSF. Pia Mfumo
huu utaondoa kabisa usumbufu kama ulikuwepo na pia utawawezesha wanachama
wetu tunaowahudumia kupata huduma kwa wakati, kwa kuwa mifumo hii ni wazi na
ufuatiliaji unakuwa rahisi.
Kuhusu sekta isiyo rasmi, Bw. Mshomba amesema Mfuko umechukua hatua
mbalimbali kuhakikisha wananchi wengi wanahamasika kujiunga na kujiwekea
akiba, ambapo kwa sasa unaendelea kutoa elimu kupitia makundi mbalimbali na
kuwaeleza faida za kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na ya baadaye.
Aidha, kuanza kwa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi
(NISS), ni utekelezaji wa mipango mahsusi iliyowekwa na Shirika la Kazi
Duniani (ILO) (Millenium Goals) ambayo pamoja na mambo mengine inataka watu
wote kuwa kwenye hifadhi ya jamii. Mshomba alifafanua kuwa NSSF imeshaweka
mikakati ya kutosha kuwafikia watu wote ikiwa ni kwa makundi na hata
mwananchi mmoja mmoja. Wananchi wote watakaojiunga na NSSF watapata Mafao na
Huduma mbalimbali kama ambavyo wafanyakazi wengine wote wanapata.
Uwepo wa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS)
utatoa fursa ya kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa makundi ambayo
hayanufaiki na huduma hizi ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa
nchi, utasaidia juhudi za Serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa
wananchi, utaongeza nguvu za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa Nchi na
mwisho utachochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla.
Bw. Mshomba amesema pia NSSF ina Skimu ya uchangiaji wa Hiari ambayo
inawahusu watumishi wote. “Natumia nafasi hii kuhamasisha na kuwataka
mchangie kupitia skimu hii kwa sababu kufanya hivyo mtajikuta mnapata kipato
cha ziada, kazi kubwa mbele yetu ni kutoa elimu ili watu wengi wapate uelewa
wa jambo hili.” amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile
amepongeza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na NSSF hasa katika kutekeleza
miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo wa kukamilisha kiwanda cha sukari
Mkulazi. Pia amepongeza NSSF kuweka mipango sasa ya kuwafikia wananchi wote
walioko katika Sekta isiyo rasmi kwani kwa kufanya hivyo sasa watu wote
tutakuwa ni wamoja na hapo baadaye wote tutanufaika, safari ya uzee ni ya
kila mmoja wetu na hivyo ni vizuri kila mmoja akifika awe na uhakika wa
kesho yake.
Balile alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waajiri wa sekta binafsi hasa
wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasilisha michango ya
wafanyakazi wao NSSF kwa wakati ili wanapostaafu waweze kulipa stahiki
zao.
“Leo tumepata bahati tumepata ushuhuda kutoka kwa wastaafu waliokuwa
wafanyakazi kutoka katika vyombo vya habari ambao ni wanufaika wa mafao ya
kustaafu na pensheni ya kila mwezi Bi. Flora Wingia na Bw. Bakari Machumu”
Aidha, wahariri wastaafu wamepewa Tuzo kwa kutambua mchango wao.
Akiwasilisha taarifa ya uendeshaji wa Mfuko, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw.
Omary Mziya amesema NSSF inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi
ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi,
kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Bw. Mziya amesema wanaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa hifadhi ya
jamii ili kuongeza uelewa wa haki ya kujiunga kwenye Skimu ya Hifadhi ya
Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS) na kuendelea kuboresha mifumo na kusogeza
huduma karibu na jamii.
“Sekta isiyo rasmi ina Watanzania takribani 11 Millioni, hawa wote
wanahitaji kinga dhidi ya majanga ambayo ni uzee na majanga mengine
yanayoweza kutokea hapa kati, kuachishwa kazi ama kufariki na
kadhalika”.
Sekta isiyo rasmi inatoa nafasi kwa Watanzania wote kujiunga na hifadhi
ya jamii, Mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi kama vile
kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali,
biashara ndogo ndogo, mama lishe/ Baba lishe, bodaboda na wasafirishaji
wengine, machinga, wanahabari wa kujitegemea.
No comments:
Post a Comment