Wadau wa waliohudhuria mafunzo ya usalama mtandaoni kwa watu wenye mahitaji maalum mkoa wa Shinyanga wakipiga picha ya pamoja
Na Kadama Malunde – Shinyanga
Watu wenye mahitaji maalumu wameipokea kwa shangwe kampeni ya "Ni Rahisi Sana," iliyoanzishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Kampeni hii ni hatua ya kihistoria inayolenga kuhimiza matumizi sahihi na salama ya mtandao, huku ikiwapa watumiaji maarifa ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni.
Kwa kutoa fursa hii ya elimu na uelewa, TCRA inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama na ujasiri wa watu wenye ulemavu na kuonyesha kwamba kila mtu ana haki ya kutumia mtandao kwa usalama lakini pia ni hatua muhimu katika kuelekea ulimwengu wa kidigitali ulio na usawa kwa wote!
Mkoa wa Shinyanga umepewa fursa ya mwanzo kabisa ya kufaidika na elimu hii, ambapo mafunzo yalitolewa tarehe 17 Oktoba 2024 ambapo Watu wenye mahitaji maalum walifundishwa kuhusu hatari za mtandaoni na jinsi ya kujilinda, jambo ambalo limeleta matumaini na ujasiri kwa wahusika.
Kampeni ya Ni Rahisi Sana imelenga kuwahimiza watanzania wote wajilinde dhidi ya uhalifu mtandaoni kwani uwepo wa mazingira salama mtandaoni utawezesha kufikia malengo ya uchumi wa Kidijiti.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga (SHIVYAWATA), Richard Mpongo (kulia anayezungumza) anasema kutokana na uelewa huu waliopewa, sasa wanaweza kutumia mtandao kwa ujasiri zaidi na kwa faida, bila hofu ya kudhurika.
“Ni muhimu sana kwa watu kama sisi kuwa na elimu hii, kwani inatupa sauti na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika jamii. Kampeni ya 'Ni Rahisi Sana' kutoka TCRA ni muhimu sana kwetu watu wenye mahitaji maalum. Kwa mafunzo tuliyopokea, sasa nina uelewa mzuri kuhusu jinsi ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni”,anaeleza Mpongo.
Anaeleza kuwa, Mafunzo hayo yamejikita katika kuwaonesha njia salama za kutumia mtandao.
“Kwa mfano, nimejifunza jinsi ya kuanzisha nenosiri salama, kutambua ulaghai na jinsi ya kukabili matukio ya unyanyasaji mtandaoni.Ninawashukuru TCRA kwa kutuletea mafunzo haya na kwa kuhakikisha hatujaachwa nyuma katika ulimwengu wa kidigitali",ameongeza Mpongo.
"Kabla ya kupata mafunzo haya nilikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kutumia mtandao. Nilikuwa na hofu ya kutokuelewa hatari zinazoweza kunikabili. Hii imenipa ujasiri zaidi kutumia mitandao ya kijamii na kuungana na watu. Nimeelewa jinsi ya kuripoti matukio ya unyanyasaji mtandaoni. Sasa naweza kushiriki mawazo yangu bila hofu, najihisi salama zaidi katika matumizi yangu ya mtandao",anabainisha Flora Nzelani ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania Mkoa wa Shinyanga,Flora Nzelani
Naye Katibu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Manispaa ya Shinyanga, Masanja William anasema kupitia mafunzo hayo, amejifunza jinsi ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni na jinsi ya kutambua hatari zinazoweza kumkabili anapotumia mtandao.
"Mafunzo haya yamekuwa na umuhimu mkubwa kwangu. Kama mtu mwenye ualbino, mara nyingi napitia changamoto za kipekee mtandaoni. Nimejifunza mbinu za kutambua ulaghai na jinsi ya kulinda taarifa zangu binafsi. Hii imenipa ujasiri zaidi kutumia mitandao ya kijamii na kushiriki mawazo yangu bila hofu.
"Mafunzo yamenisaidia sana nilikuwa nasumbuliwa na SMS za matapeli , sasa naweza kutoa taarifa kuhusu mtu anayetaka kunitapeli kwa kutuma namba yake kwenye namba 15040 ili kukomesha tabia za wezi wa mtandao. Yameniepusha kuingia kwenye hasara mfano nikitoa neno la Siri au kubonyeza viunganishi nisivyovijua", ameongeza.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Ansila Joackim Materu anaeleza kuwa, elimu ya kujilinda mtandaoni ni hatua muhimu katika kuwasaidia watu wenye ulemavu kujitambua na kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni.
No comments:
Post a Comment