Na Mwandishi Maalum, Singapore
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mifumo thabiti ya matumizi ya Nishati Jadidifu ili kukidhi mahitaji ya Nishati kwa nyakati zote.
Dkt Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 22, 2024 nchini Singapore wakati akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa uimarishaji wa mifumo kwa ajili ya matumizi ya Nishati Jadidifu kwenye mkutano wa Jukwaa la Juu la viongozi wanachama wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Nishati Jadidifu (IRENA) ikiwa ni sehemu ya mkutano wa kimataifa wa Wiki ya Nishati inayoendelea nchini Singapore.
Amesema sera za uwazi zitasaidia ukuaji wa sekta ya Nishati na kuvutia fursa kwa wawekezaji.
‘’Nipende kutoa witio kwa wanachama wenzangu wa IRENA kuhakikisha tunaweka sawa masuala ya kisiasa duniani, mabadiliko ya bei kwenye soko la Nishati, vita vya kibiashara, uhaba wa rasilimali kwani yana mchango mkubwa kwenye kuathiri mifumo ya usambazaji wa Nishati’.’ Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Tanzania kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya Nishati Jadidifu kwa kuwa rasilimali hiyo ipo ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya vyanzo vya umeme na kuwaalika wawekezaji kuwekeza nchini kwenye miradi hiyo.
Awali akizungumza kwenye jukwaa hilo la IRENA, Waziri wa Utawala,Viwanda na Biashara wa Singapore Dkt. Tan See Leng amesema, nchi wanachama wameweka mikakati ya kuhakikisha wanaongeza kwa takriban asilimia 90 matumizi ya Nishati jadidifu ili kulinda usalama wa nchi zao na kupunguza gesi ya ukaa yenye athari kwa mazingira na pia kurahisisha upatikanaji wa Nishati safi ya kupikia.
Ametaja masuala mengine ambayo yatapewa kipaumbele ni pamoja na kuhakikisha nchi wanachama wanaunganishwa na wanachama kwenye mifumo ya umeme ya Gridi kwa ajili ya kuuziana umeme, kuhakikisha Nishati ya umeme inapatikana kwa watu wote sambamba na kuongeza mahitaji ya umeme kwa nchi wanachama na kuimarisha mifumo na uimara wa Gridi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa IRENA, Francesco La Camera, amesema mahitaji ya umeme yameongezeka duniani na kufikia Terabaiti 2.3, hivyo nchi wanachama takriban 133 wanachama wa IRENA wamekubaliana kuwekeza zaidi kwenye Teknolojia, Sera na utafutaji wa masoko na uboreshaji wa miundombinu ili kufikia lengo na tayari IRENA imetoa msaada wa kitaalamu kwa wanachama 96 kwa ajili ya kusaidia maboresho hayo.
Mjadala huo ullijadili pia masuala ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuboresha Gridi na uunganishaji wa wateja kwa nchi wanachama.
Katika Mkutano huo wa Wiki ya Nishati Singapore, Tanzania inawakilishwa na Wadau kutoka wizara ya Nishati, EWURA na TANESCO.
No comments:
Post a Comment