Na WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 14 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya mafunzo ya kibingwa na ubingwa bobezi kwa wataalamu wa afya, ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 3.0, sawa na asilimia 28 zaidi ya bajeti iliyotengwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 ya Shilingi Bilioni 10.95.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameyasema hayo leo oktoba 21, 2024 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya mpango wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuongeza wataalamu Bingwa na Bobezi wa afya nchini, kwa mwaka 2024/25 “SAMIA HEALTH SPECIALIZATION SCHOLARSHIP PROGRAM 2024/25”, katika ukumbi wa Wizara jijini Dodoma.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25 fedha zilizotengwa zitatumika kugharamia mafunzo ya wataalamu 544 kwa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na wataalamu wengine 47 kwa utaratibu wa seti na wataalamu 829 wanaoendelea na mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi, wataendelea kupata ufadhili kupitia fedha hizo,” amesema Waziri Mhagama.
Utaratibu huu wa kusomesha wataalam kwa seti utasaidia katika upatikanaji wa wataalam wanaofanya kazi katika mnyororo wa utoaji wa huduma za kibingwa kwa pamoja. Kwa mfano; Wataalamu watakaosomeshwa kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu ya figo kikamilifu katika set ni kama ifuatavyo; Daktari Bingwa wa Upasuaji Figo, Daktari Bingwa wa matibabu ya Figo, Daktari Bingwa wa utoaji dawa ya Usingizi kwa wagonjwa wa Figo.
Waziri Mhagama amesema lengo la mpango huu ni kuhakikisha wanasomesha wataalamu bingwa na bobezi wasiopungua 300 kila mwaka kwa kupitia mpango maalumu wa Serikali wa “Samia Health Specialization Scholarship Program”.
Aidha Waziri Mhagama amesema jitihada hizo za kusomesha wataalam zinalenga kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa huduma bora za afya, kupunguza rufaa za nje ya nchi huku lingine ikiwa ni kupunguza gharama za Serikali na wananchi.
“Mwaka huu wa fedha 2024/25, Wizara ilipokea jumla ya maombi ya ufadhili 948 nchi nzima, kati ya hao waombaji wa jinsia ya kike ni 353 na kiume ni 595 , huku waombaji 771 wakikidhi vigezo vya kufadhiliwa na waliochaguliwa kwa ajili ya ufadhili wakiwa 544, jinsia ya kiume ni 338 na kike ni 206. Kati ya hao waliopata ufadhili wa kusoma vyuo vya ndani ya nchi nonje ya nchi ni n 517 (95%) na nje ya nchi 27 (5%),” amesema Waziri Mhagama.
Hata hivyo Waziri Mhagama amesema wizara imezingatia vipaumbele muhimu vya kisekta kama ubobezi katika ngazi mbalimbali za huduma ,ikiwa ni pamoja na taaluma za watoto wachanga , afya ya akili, magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kama vile moyo , matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu, huduma za utengamao na tiba shufaa , pia kipaumbele kwa maeneo yenye uhaba mkubwa wa wataalamu bingwa kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia.
“Nichukue fursa hii kuendelea kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Afya hususani katika kuendeleza wataalamu bingwa na bobezi ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata matibabu ya kibingwa na kibobezi yanayotolewa na wataalamu wetu wa ndani,”amesema Waziri Mhagama.
No comments:
Post a Comment