Mkurugenzi Msaidizi wa kutoka Ofis ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Huduma za Lishe Bw. Luitfrid Nnally amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la hamasa kwa wananchi katika kutekeleza Afua muhimu za Lishe tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Lishe na kupelekea kupungua kwa matatizo yatokanayo na upungufu wa lishe bora kwa kiasi kikubwa.
Ameyasema hayo Katika Mkutano wa Nane wa Tathimini ya Mkataba wa lishe na Kutambulisha Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika Afya ya Mama na Mtoto (TMCHIP) uliofanyika katika ukumbi wa Jiji Mtumba, Jijini Dodoma.
Mkataba huo wa lishe ambao Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais alimwagiza Mh. Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI asaini Mkataba na Wakuu wote wa Mikoa ili kuimarisha usimamizi katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kupunguza changamoto ya Lishe na athari zake.
Bw. Nnally amesisitiza kuwa matatizo mbalimbali ya Lishe ni miongoni mwa changamoto zinazopunguza kasi ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo katika Taifa letu hivyo jitihada kubwa zinahitajika ili kuyatatua ikiwa ni pamoja na kutoa elimu, Kwani Huduma za lishe zinalenga kuimarisha rasilimali watu (Human Capital Development) ambao ni mtaji wa kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na maradhi, umasikini na ujinga na hivyo kuongeza uwezo wa Kukuza Uchumi katika Taifa.
Mkutano huo ambao Mgeni wake Rasmi alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa Umehudhuliwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga wa Kuu wa Mikoa na wa Wa halmashauri na Maafisa lishe wa Mikoa.
No comments:
Post a Comment