RC MACHA AZITAKA HALMASHAURI MKOANI SHINYANGA KUWASHIRIKISHA WAZEE KATIKA VIKAO NA MIKUTANO YOTE. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 26 September 2024

RC MACHA AZITAKA HALMASHAURI MKOANI SHINYANGA KUWASHIRIKISHA WAZEE KATIKA VIKAO NA MIKUTANO YOTE.



9f
Na. Paul Kasembo, USHETU.


MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amezitaka Halmashauri zote mkoani Shinyanga kuhakikisha zinawashirikisha na kuwaalika Baraza la Ushauri la Wazee katika maeneo yao ili waweze kushiriki katika vikao na mikutano yote ikiwa ni sehemu ya kutambua, kuwaenzi na kuthamini uwepo na mchango mkubwa katika Taifa hili.


RC Macha ameyasema haya leo tarehe 26 Septemba, 2024 alipoongoza Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ambapo Kimkoa yamefanyika Kijiji cha Igunda kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wazee akiwemo Makamu Mwenyekiti Baraza la Wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Richard Mihayo, Katibu wa Baraza Mkoa wa Shinyanga Mzee Anderson Lymo, Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani na wajumbe wote kutoka katika Halmashauri zote sita za Mkoa huku msisitizo zaidi ukiwekwa kwenye kujitunza, kujipenda na kushiriki shughuli za kijamii.




"Nitumie nafasi hii kuzitaka Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kuwa viongozi kutoka Baraza la Ushauri la Wazee wanashirikishwa kikamilifu katika vikao na mikutano yote katika maeneo yao ikiwemo katika Mabaraza ya Waheshimiwa Madiwani ili tuwaenzi, tutambue na kuthamini michango yao katika Taifa" amesema RC Macha.




Pamoja na kupokea risala ya wazee, RC Macha amewapongeza sana huku akiwakumbusha kuwa kuanzia tarehe 11 - 20 Oktoba, 2024 ni kipindi cha kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, na itakapofika tarehe 27 Novemba, 2024 wajitokeze kupiga kura ili kuchagua viongozi ambao watakuwa na tija kwao ukizingatia kuwa wao ni wazee huku akihamasisha pia kugombea nafasi hizo kwani ni haki yao pia.




Kwa upande wake Mhe. Cherehani amesema kuwa, ofisi yake inatambua na kuthamini sana uwepo wa wazee katika Jimbo la Ushetu na kwamba yeye mwenyewe amekuwa akishirikiana nao wakati wote ambapo mpaka sasa amefanya mikutano takribani 272 katika vijiji vyote 112 na Kata 20 za Ushetu ambapo amekuwa akishirkiana nao vema huku akiwakumbusha mema mengi ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyafanya kwa Wanaushetu.




Awali akisoma Risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Shinyanga amesema kuwa wao kama wazee wataendelea kuitumia Kauli Mbiu hii kuelimisha vijana ili waelewe dhamira njema ya Serikali ya kuwatengenezea mazingira rafiki ya kuzeeka kwa heshima sasa hivi kwani wao ni vijana na wazee wa kesho ukizingatia Uzee na Kuzeeka, hakukwepeki.

Mkoa wa Shinyanga unaadhimisha Siku ya Wazee duniani ikiwa na takribami wazee 68,632 kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso