NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL
Mtu mmoja mkazi wa Mwime-Makungu Wilayani Kahama amezua taharuki kwa wakazi wa mtaa huo baada ya kukutwa na jeneza karibu na shamba lake huku akiwazuia watu kupita eneo hili hali iliyowapelekea kuwa na hofu kwani mauaji yameongezeka.
Mtu huyo aliyetambulika kwa jina la Kumalija Budeba (55) ayedaiwa kuwa ni Mganga wa Kienyeji amezua taharuki hiyo baada ya Vijana waliokuwa wakichunga Mifugo kuliona Jeneza hilo kisha kutoa taarifa kwa Uongozi wa Serikali ya Mtaa ambao walitoa taarifa Polisi.
Kumalija amekiri kufahamu uwepo wa Jeneza hilo ambalo lilikuwa likitumiwa na Msanii wa Nyimbo za asili Idd Masempele ambaye alimwita nyumbani kwake kwa ajili ya kumfundisha kijana wake sanaa ya Muziki wa asili na alikuwa analitumia katika matamasha yake.
"Jeneza hili tulikuwa tunalitumia kwenye matamasha ya Muziki wa asili tangu Mwaka jana Msaanii wangu Idd Masempele aliliacha hapa baada ya kumaliza matamasha ya Ngoma za asili leo nimeshangaa kuona kundi la Watu wakivamia nyumba yangu wakihoji juu ya uhalali wake,kwani niliambia anakibali toka Manispaa ya Kahama,"alisema Budeba.
Kiongozi wa Walinzi wa Jadi (sungusungu) wa Mtaa huo, Someke John amesema walilazimika kufika eneo la tukio ambapo walifungua jeneza hilo ili kujirizisha kama kuna mwili wa binadamu lakini walikuta jeneza liko tupu
"Tulipomhoji Kumalija alikiri kufahamu uwepo wa Jeneza hilo ambalo alikuwa akilitumia katika shughuli za Sanaa,pia alitueleza kuwa Msaanii wake anaitwa Idd Masempele alikuwa analitumia katika Matamasha yake ya Muziki wa asili alilitelekeza katika eneo hili Mwezi wa Saba Mwaka huu,"alisema John.
Nae Martha Mihambo Mkazi wa Mtaa wa Mwime amsema Jeneza hilo limewashangaza kwani katika uwasilishaji wa sanaa ya Muziki wa nyimbo za asili hakuna kipengele cha kutumia jeneza hivyo Kumalija alipaswa kuwa na kibali cha kulitumia na kuliweka nyumbani ili kutoibua maswali kwa Wananchi.
Akijibu hoja za kibali cha Jeneza hilo Afisa Utamaduni Manispaa ya Kahama Felix Ntibabara amesema kuwa hawajawahi kutoa kibali cha Matumizi ya Jeneza kwa ajili ya shughuli za sanaa za asili,na katika uwasilishaji wa maudhui ya nyimbo za asili ni kosa kutumia aina hiyo ya sanaa.
Kwa Mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Kennedy Mgani amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa Kumalija Budeba na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kujua uhalali wake na Jeneza hilo lipo kituo cha Polisi Kahama.
No comments:
Post a Comment