Na WAF, Hanang - Manyara
Kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia imefanikiwa kumfanyia upasuaji Bi. Natalia Bilauri Mwenye umri wa miaka 53 mkazi wa kijiji cha Wamha aliyekuwa na tatizo la uvimbe kwenye nyonga kwa takribani miaka miwili.
Hayo yamesemwa Septemba 26, 2024 na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Rais Samia Dkt. Amri Mabewa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida aliyepo kwenye kambi ya Matibabu ya Madaktari bingwa wa Rais Samia kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Hanang mkoani Manyara.
Dkt. Mabewa amesema uvimbe huo unahisiwa kuwa ni saratani hivyo baada ya kumfanyia upasuaji wamechukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Uvimbe huu ulianzia mguuni na aliktakiwa kufanyiwa upasuaji lakini baadae ukazalisha uvimbe mwengine kwenye nyonga aliodhani ni jibu na kuutumbua na kutoa damu nyingi kwa muda.”Amesema Dkt. Mabewa na kuongeza kuwa
“Wakati tupo kwenye upasuaji tulipokea dharura ya kijana aliyepata ajali na kuumia zaidi maeneo ya kichwani na usoni na ametoka vizuri na bado tunaendelea kumtazama kama atahitaji huduma zaidi tunaweza kupa rufaa”
Aidha Dkt. Mabewa ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika hospitali zote za halmashauri nchini kwa kuwapatia vifaa tiba vya kisasa na majengo ya kutosha jambo ambalo linarahisisha utendaji kazi kwa kambi hizo za madaktari bingwa .
“Nitoe wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa na uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na serikali yao na kwa upande wetu sisi watumishi wa afya tuendelee kujifunza ili kuweza kutoa huduma bora kwa watanzania”
Kwa upande wake Bi. Natalia Bilauri amesema alifika hospitalini hapo mara baada ya kusikia ujio wa madaktari bingwa wa Rais Samia na amewashukuru kwa huduma zao bora na utu wao.
No comments:
Post a Comment