Chanzo cha picha,AFPMaelezo ya picha,Freeman Mbowe
Viongozi mbalimbali wamejitokeza katika mazishi ya kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema, Ali Kibao aliyedaiwa kutekwa siku ya jumamosi na baadaye mwili wake kupatika katika eneo laUnunio, kaskazini mwa Dar es Salaam.
Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa mambo ya ndani nchini humo, Hamad Masauni ambaye amewahakikishia waombelezaji kuwa serikali haitalinyamazia jambo hili
“Mheshimiwa raisi amesononeshwa na kuumizwa sana na tukio hili, pamoja na serikali nzima, ni jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi yetu ambayo tumekuwa tukijivunia usalama na amani.
Waziri Masauni amesema tukio hili kama serikali hawataliacha lipite, kwani maelekezo ya Rais ya kufanyiwa uchunguzi yameanza kutekelezwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Chadema, Freeman Mbowe, amemtaka Waziri Masauni kuwasilisha rai ya waombolezaji kwa Rais Samia ya kuunda tume ya kijaji kuchunguza matukio yote ya aina hii kwani Rais ndiye mwenye mamlaka hiyo.
“Wote tumesikia kauli ya Rais ambayo inaelekeza vyombo vile vile ambavyo ndio watuhumiwa namba moja wakajichunguze wenyewe tunaona hilo haliwezekani, hii nchi haitarekebika”
“Tunaamini hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kusaidia ikaundwa tume ya kijaji ya kimahakama ikafanya uchunguzi wa jambo hili ili sisi wengine ambao inawezekana tuna baadhi ya Ushahidi ambao hatutakuwa tayari kuutoa polisi tutautoa kwa tume hii.
Mwanachama na mjumbe wa kamati kuu Chadema, Godbless Lema ameelezea kusikitishwa na kifo cha mwanachama mwenzake .
“Niliposikia amekamatwa nilijua ni matukio ya kawaida kabisa ambapo pengine kesho yake tungeweza kumuona, lakini taarifa ya jana nilipoisikia Maisha yangu yamekuwa magumu sana” Alisema Godbless Lema
Ali Kibao amezikwa leo, nyumbani kwake mkoani Tanga.
Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema alichukuliwa jioni ya Septemba 6, 2024jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi na mwili wake kupatikana jana Jumapili Septemba 8, 2024 eneo la Ununio, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment