Na. Paul Kasembo, SHY RS.
KATIBU Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amefungua Mkutano wa Kuwasilisha na Kujadili Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Mkoa wa Shinyanga huku akwaisisitiza wajumbe kujadili kwa kina na kwa maslahi mapana ya Wanashinyanga na Taifa kwa ujumla wake.
CP. Hamduni ameyasema haya leo tarehe 3 Septemba, 2024 katika mkutano huu ambao umefanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo umeratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).
"Pamoja na pongezi kwa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, lakini pia niwaombe na kuwasisitiza wajumbe kushiriki kikamilifu katika mkutano huu ambao unao maslahi mapana ya Wanashinyanga na Taifa kwa ujumla," amesema CP. Hamduni.
Akiwasilisha dhumuni la mkutano huu, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kutoka (NLUPC) ndg. Jonas Nestory Masingija amesema kuwa uwepo wa mkutano huu unakwenda kupata maoni na mapendekezo ya wataalam ambao utaleta tija na kuona namna ya kutumia vema ardhi kuongeza thamani ya vyote vitokanavyo na ardhi ili kukuza uchumi na kuongezeka kwa kipato cha wananchi wa Shinyanga na Taifa huku akisisitiza kuwa miaka 20 ijayo Shinyanga inakwenda kubadilika kabisa.
"Tafiti zinaonesha, miaka 20 ijayo kuanzia sasa Mkoa wa Shinyanga unakwenda kuwa ni kitovu cha usindikaji wa mazao ya mifugo, chakula na senta kubwa ya madini", amesema Nestory.
Aina za ardhi zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga ni ardhi ya jumla 18% ambayo ni Manispaa ya Shinyanga na Kahama Manispaa, huku ikitajwa kuwa ardhi iliyo kubwa ni ardhi ya vijiji yenye 75% na ardhi ya hifadhi ni 6% ikijumuisha msitu wa Ushetu Ubagwe, Nindo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Mkweni uliopo sehemu ya Manispaa ya Kahama.
No comments:
Post a Comment