Binti mwenye umri wa miaka 22 na mkazi wa kijiji cha Shilabela, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Naomi Robert Luhedeka amefariki dunia kwa kujinyonga ndani ya chumba chake cha kulala.
Tukio hilo limetokea jana saa saba mchana, na taarifa za kifo chake zimepokelewa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Emmanuel Magadula majira ya saa nane mchana.
Akizungumza na Misalaba Media, Mwenyekiti Magadula ameelezea namna alivyopokea taarifa za tukio hilo ambapo amesema binti huyo alikuwa na tatizo la sikoseli tangu utotoni.
"Taarifa ya kifo cha huyo binti nimezipokea muda wa saa nane mchana nikiwa nyumbani yule binti amejinyonga ndani ya chumba chake alipokuwa akiishi na mama yake pamoja na bibi yake, Binti huyo alikuwa na tatizo la sikoseli tangu utotoni." Amesema Mwenyekiti Magadula
Mwenyekiti ameongeza kuwa, mama wa marehemu alikuwa akifyatua matofali akiwa na watoto wake wengine, wakati ambapo Naomi aliwaambia anakwenda kulala, dakika chache baadaye dada yake ambaye anasoma chuo alimuomba mama yake akajiadae kwa ajili ya kwenda shule ambapo alipoingia ndani alikuta Naomi tayari amejinyonga kwa kutumia mtandio kwenye kenchi ndani ya chumba chake.
Mwenyekiti ameeleza kuwa taarifa zilifikishwa kwa polisi ambao walifika eneo la tukio, kupima mwili wa marehemu na kuruhusu taratibu za mazishi kuendelea.
Mazishi ya binti huyo yamefanyika leo Septemba 19, 2023 majira ya saa nane mchana katika kijiji cha Shilabela.
Mwenyekiti Magadula ametoa wito kwa wananchi ambapo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza kuwa na utaratibu wa kwenda kwenye nyumba za ibada ili kupata mafundisho ya dini.
"Naomba wananchi wawe na ustaarabu, na kikubwa zaidi watu wajiunge na kanisani inawezekana msongo wa mawazo umempelekea binti huyo kufanya maamuzi hayo, hivyo ni muhimu kupata mafundisho ya dini."amesema Magadula
Misalaba Media imefanya jitihada za kumpata Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa ACP. Kennedy Mgani, ili kupata taarifa rasmi kuhusu chanzo cha tukio hilo haijafanikiwa.
No comments:
Post a Comment