WAZAZI PELEKENI VIJANA WENU SHULE - MAJALIWA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 23 August 2024

WAZAZI PELEKENI VIJANA WENU SHULE - MAJALIWA



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi wahakikishe vijana wao wanakwenda kusoma kwenye shule za sekondari kwani bila elimu hawawezi kufika mbali.


“Wazazi wenzangu hakikisheni vijana wenu wanaenda shule. Hatuwezi kufika mbali kama vijana wetu hawaendi shule. Tunajenga shule kila mahali, tunataka maeneo yote yawe na shule,” alisema.


Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alitoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Agosti 22, 2024) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambiranje, Ruangwa mkoani Lindi.


Akielezea hatua iliyofikiwa kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu alisema Wilaya ya Ruangwa imepiga hatua kwenye sekta za elimu, maji na afya ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.


Alisema wilaya hiyo ina shule tatu za wasichana pekee ambazo ni Liuguru, Ruangwa Girls na Lucas Malia. “Vilevile tumefanikiwa kujenga shule za sekondari zenye kidato cha tano na sita ambazo ni Ruangwa, Mbekenyera, Nkowe, Lucas Malia na Hawa Mchopa. Shule ya sita ya Mandawa itakamilika hivi karibuni,” alisisitiza.


Akielezea utekelezaji kwenye sekta ya maji, Waziri Mkuu alisema vijiji vyote 90 vya wilaya vilichimbiwa maji kupitia taasisi ya GAIN lakini kwa sasa hayatoshi. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwajulisha kwamba Serikali imetoa sh. bilioni 49 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka Nyangao ambao utavinufaisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 29 vya wilaya ya Nachingwea.


Kuhusu umeme, alisema kwamba laini zimeshaenda kwenye kila kijiji na kwamba Serikali hivi sasa inashughulika kuweka umeme kwenye ngazi ya vitongoji. “Leo hii hakuna kijiji kisichokuwa na umeme.”


Kuhusu barabara, alisema kuna changamoto ya barabara kufika katika kijiji cha Mtondo ambayo tayari iko kwenye mpango wa ujenzi. “Kuna barabara ya kutoka Mandawa Chini hadi hapa, Nanjalu hadi hapa, Nambiranje hadi hapa na kutoka Namiyenje hadi hapa.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso