WAWEKEZAJI WAZAWA WAMPA KONGOLE RAIS SAMIA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 4 August 2024

WAWEKEZAJI WAZAWA WAMPA KONGOLE RAIS SAMIA





NA ANTHONY SOLLO NYANG’HWALE



WAKATI Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ikitimiza miaka mitatu wachimbaji wadogo wamesema Serikali imeweka juhudi kubwa katika kuboresha Sekta ya Madini nchini.




Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake,Meneja wa Kampuni ya DOMEIN inayojishughulisha na shughuli za uchenjuaji wa Madini katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bi Sabina Mpejiwa Makune amesema,katika kipindi hiki Serikali imefanikiwa kuimarishana kuboresha Sheria na Kanuni zinazowahusu wachimbaji wadogo wa Madini na kuhakikisha wanapata Haki zao na wanachangia pato la Taifa ili kukuza Uchumi.



Bi Sabina Mpejiwa amebainisha kuwa,kupitia Serikali,wao kama wachimbaji wadogo wamenufaika na awamu ya Sita hasa kwa kupata ufadhili na Mikopo kutoka Taasisi za Fedha huku Serikali ikisaidia kuboresha Vifaa na Teknolojia inayotumika katika kiwanda chao cha kuchakata Madini.




Pichani ni mmoja wa wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchenjua Dhahabu cha Kampuni ya DOMEIN iliyoko Halmashauri ya Nyang'hwale Mkoani Geita kama alivyokutwa akifanya shughuli zake katika Kiwanda hicho Picha na Antony Sollo
Pichani ni Bi Sabina Mpejiwa Makune ambaye ni Meneja wa Kiwanda cha uchenjuaji wa Madini ya Dhahabu cha DOMEIN kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale Mkoani Geita.













Hayo hapo juu ni matanki yanayotumika katika Kiwanda cha kuchenjulia Dhahabu katika Mgodi wa DOMEIN Picha na Antony Sollo.












Kuhusu utoaji wa Elimu na Mafunzo Mpejiwa amesema kupitia Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanikisha kuendesha Programu za Mafunzo na Elimu kwa wachimbaji ili kuwaongezea ujuzi na maarifa ya kisasa katika uchimbaji na usalama kazini.



Kwa upande wa uboreshaji wa Miundombinu ya barabara Mpejiwa ameiomba Serikali kuhakikisha inafanyia kazi mapungufu yaliyoko katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji huku akiitaja Migodi kama Isonda Ifugandi,Mahagi na maeneo mbalimbali ambako ndiko kiwanda hicho kinategemea kupata Malighafi kwa ajili ya uchakataji wa Madini.



Aidha Meneja huyo ambaye ni mwanadada Mtanzania mbobevu wa Mitambo yta uchenjuaji wa Madini ameeleza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita zimewafikisha mbali katika mafanikio na kuongeza kuwa Sekta ya Uchimbaji Madini imetoa mchango mkubwa kwa ukuaji wa Uchumi nchini Tanzania.



Akizungumzia uzalishaji wa Madini ya Dhahabu Mpejiwa amebainisha kuwa wachimbaji wadogo huchangia kati ya 30% hadi 40% ya uzalishaji wote na kuongeza kuwa mchango wa wachimbaji wadogo umeendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa Madini ya Dhahabu Sokoni.



Meneja huyo amebainisha kuwa,katika upande wa Ajira,Sekta ya Uchimbaji wa Madini imekuwa kinara kwa kuajiri maelfu ya watu moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kuongeza kuwa Sekta hii imekuwa chanzo kikuu cha Ajira kwa Vijana wahitimu wa Sekta ya Madini.

Hata hivyo Meneja Mpejiwa ameeleza kuwa kupitia Kodi na Ada mbalimbali,wachimbaji wadogo huchangia pato la Serikali kwa kulipa Kodi na Mirabaha pamoja na Leseni za uchimbaji.



Kuhusu Maendeleo ya Jamii,Meneja Mpejiwa amesema wachimbaji wadogo wamefanikiwa kuchangia maendeleo ya jamii kwa kuboresha huduma za Msingi kama Elimu,Afya, na Miundombinu katika maeneo ya uchimbaji wa Madini.










Meneja huyo wa Kampuni ya uchenjuaji wa Madini DOMEIN amesema kuwa wachimbaji wa Madini wamefanikisha pia kupunguza Umaskini kwa kutoa fursa za kujipatia kipato kwa Familia nyingi,hasa watu wanaojihusisha na uchimbaji wa Madini ambao leo wanaweza kujivunia Sekta hii ya uchimbaji.



“Mchango wa Sekta ya Madini ni mkubwa,na unahitaji kuendelezwa,ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata misaada na fursa za kuboresha shughuli zao za uchimbaji na kuwahakikishia Mazingira mazuri ya usalama kazini”amesema Meneja Mpejiwa.



Katika hatua nyingine Meneja wa Kiwanda cha kuchakata Madini DOMEIN Elution Plant Sabina Mpejiwa Makune amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu pamoja na wasaidizi wake akiwemo Waziri wa Madini Antony Mavunde,Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe Mhandisi Jeremia Hango na Timu nzima ya Wataalamu kwa namna wanavyotoa ushirikiano wao kwa wawekezaji wazawa.



“Napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake akiwemo Waziri wa Madini Anthony Mavunde,Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe Mhandisi Jeremia Hango na Timu nzima ya Wataalamu kwa namna wanavyotoa ushirikiano wao kwetu kama wawekezaji wazawa”.

MWISHO.




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso