Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Laki Moja, Bi. Anascholastica Ndagiwe akisoma tamko la Kikundi kazi cha kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (Shinyanga EVAWC Working Group) kulaani kitendo cha kikatili alichofanyiwa msichana kutoka Dar-es-salaam, Wilaya ya Temeke, Mitaa ya Yombo Dovya na kisha kusambazwa katika mitandao ya kijamii.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kupitia Kikundi kazi cha kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (Shinyanga EVAWC Working Group) wametoa tamko la kulaani kitendo cha kikatili alichofanyiwa msichana kutoka Dar-es-salaam, Wilaya ya Temeke, Mitaa ya Yombo Dovya na kisha kusambazwa katika mitandao ya kijamii tangu tarehe 03/08/2024.
Akisoma tamko kwa niaba ya Kikundi hicho, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Laki Moja mkoa wa Shinyanga, Bi. Anascholastica Ndagiwe amesema kwa kauli moja wanalaani kitendo hicho cha kikatili kinachodaiwa kufanywa na vijana watano wanaosemekana kuwa ni Askari wa kutoka katika moja ya majeshi nchini.
'Na vile vile inasemekana kuwa video hii imesambazwa kwa maelekezo ya kiongozi wao ambaye pia ni askari aliyewaagiza wafanye kitendo hicho cha kikatili kama adhabu kwa binti huyo kwa kosa la kuwa na mahusiano na mume wake',amesema Ndagiwe.
"Shinyanga EVAWC Working Group kwa umoja wetu tunalaani vikali kitendo hiki kwani ni kinyume na sheria za nchi kama ilivyoelezwa kupitia sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyorekebishwa mwaka 2022 inayoainisha makosa ya kingono na adhabu zake ikiwa ni pamoja na matendo ya ubakaji (gang rape) yanayotajwa kwenye kifungu cha 131A na kifungu cha 151, kinachoeleza kuwa mtu yeyote atakayefanya kitendo cha ulawiti kwa mwanaume mwenzake, Mwanamke au mtoto atakuwa ametenda kosa na atawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na adhabu kali",ameesema
Ameeleza kuwa Adhabu inaweza kuwa kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka thelathini (30) kulingana na mazingira ya kosa hilo hivyo wana Shinyanga EVAWC Working Group wanatafsiri kitendo hiki kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kutoa rai kwa vyombo vyote vya kisheria vinavyohusika kutumia mikakati yote ya kuwachukulia hatua wahusika wote waliofanya kitendo hiki cha kinyama na ambacho hakikubaliki kwenye jamii.
"Na vile vile tunakemea vikali picha na video hii kuendelea kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwasababu zinazidi kumfedhehesha binti huyo aliyefanyiwa kitendo hiki. Tunatambua video hii iko kinyume na maadili, mila na desturi, miiko ya kitanzania na ukiukwaji wa sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015.
Aidha, tunatoa rai kwa taasisi zote zinazojihusisha na utoaji wa huduma za msaada wa kisaikolojia na huduma zingine za kibinadamu kuona namna wanavyoweza kuhakikisha binti huyu anasaidiwa awe sawa baada ya madhila yaliyompata",ameongeza
"Tunasema haya kwani katika mijadala yote na matamko rasmi ya mamlaka za serikali yanayotolewa tangu kuanza kwa sakata hili hatujasikia namna ambayo binti huyu amepatiwa huduma kama ambavyo miongozo ya utoaji huduma kwa madhura wa vitendo vya ukatili inavyoelekeza. Tunaamini katika weledi wa taasisi zote husika zinazoshughulika na jambo hili kuwa zitatekeleza majukumu yao kwa wakati na haki itatendeka ikiwemo kukomesha kabisa vitendo kama hivi kutokea tena",ameeleza.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Laki Moja, Bi. Anascholastica Ndagiwe akisoma tamko la Kikundi kazi cha kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (Shinyanga EVAWC Working Group) kulaani kitendo cha kikatili alichofanyiwa msichana kutoka Dar-es-salaam, Wilaya ya Temeke, Mitaa ya Yombo Dovya na kisha kusambazwa katika mitandao ya kijamii tangu tarehe 03/08/2024
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake Laki Moja, Bi. Anascholastica Ndagiwe akisoma tamko la Kikundi kazi cha kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (Shinyanga EVAWC Working Group) kulaani kitendo cha kikatili alichofanyiwa msichana kutoka Dar-es-salaam, Wilaya ya Temeke, Mitaa ya Yombo Dovya na kisha kusambazwa katika mitandao ya kijamii tangu tarehe 03/08/2024
Sehemu ya Wana Kikundi kazi cha kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga (Shinyanga EVAWC Working Group)
No comments:
Post a Comment