RAIS SAMIA AWEKA HISTORIA KUBWA UZINDUZI WA SGR - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 1 August 2024

RAIS SAMIA AWEKA HISTORIA KUBWA UZINDUZI WA SGR



*Rais Samia aweka historia kubwa uzinduzi wa SGR

* Samia anajenga kilomita 1,800 za reli ya SGR, huku Awamu ya 5 ikianzisha ujenzi wa kilomita 721

* Tanzania sasa inaelekea kuwa na reli ndefu kuliko zote kwenye bara zima la Afrika

* Rais Samia ametimiza ndoto za marais wote waliopita tangu Tanzania ipate uhuru

* Asilimia 86 ya reli yote ya SGR ya Tanzania inajengwa chini ya utawala wa Rais Samia



Agosti 1, 2024

Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka historia leo kwa kuzindua rasmi huduma za usafiri wa treni ya kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na makao makuu ya nchi Dodoma na hivyo kutimiza ndoto za marais wote waliomtangulia tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.



Ndoto ya kuiunganisha Dar es Salaam na Dodoma kwa reli ya kisasa ya SGR ilianza tangu enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Awamu ya Kwanza.


Naye Rais wa Awamu ya 2, Ali Hassan Mwinyi, aliendeleza ndoto hiyo na kupokewa kijiti na Rais Benjamin Mkapa wa Awamu ya 3.


Chini ya uongozi wa Rais Mkapa, nchi tatu za wakati huo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),Tanzania, Kenya na Uganda, ziliweka makubaliano ya kujenga reli ya SGR kuunganisha mataifa hayo.


Rais wa Awamu ya 4, Jakaya Kikwete, naye aliendeleza ndoto hiyo kwa serikali yake kufanya upembuzi yakinifu (feasibility study) ya ujenzi wa reli ya SGR.


Rais wa Awamu ya 5, John Magufuli, alionesha uthubutu kwa kuanza ujenzi wa kilomita 721 za reli ya SGR.


Alipoingia madarakani Machi 2021, Rais wa Awamu ya 6, Samia Suluhu Hassan, aliendeleza ujenzi wa reli ya SGR kwa kasi ya ajabu na kuongeza kilomita nyingine 1,800



Jumla ya kilomita 2,102 za reli ya SGR zinazoendelea kujengwa nchi nzima, huku kilomita 1,800 zikiwa zinajengwa na Rais Samia.


Hii inamaanisha kuwa asilimia 86 ya reli yote ya SGR ya Tanzania inajengwa chini ya uongozi wa Awamu ya 6 ya Rais Samia.


Ujenzi huu mkubwa unaifanya Tanzania kuwa nchi ya Afrika yenye SGR ya urefu mkubwa zaidi barani humo.


Ujenzi unaoendelea wa reli ya SGR kwa kasi kubwa unatarajiwa kufika hadi kwenye mikoa ya mipakani na kuiunganisha Tanzania na nchi jirani, hivyo kukuza fursa za kilimo, biashara na uchumi.


Inatarajiwa kwamba ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi mkoa wa Mwanza utakamilika mwaka 2026, wakati reli ya Dar es Salaam hadi Kigoma itakamilika mwaka 2027, kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Reli la Tanzania (TRC).


Kukamilika kwa reli ya SGR kutafungua biashara ya mizigo na abiria kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi nchi jirani.


Huduma ya usafiri wa abiria kupitia treni ya kasi ya umeme ya SGR pia itaongeza biashara kati ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma na nchi jirani.


Thamani ya viwanja vya Dodoma na Morogoro inatarajiwa kuongezeka kwa kasi kutokana na usafiri wa SGR kwani sasa hivi mtu anaweza kutoka Dar es Salaam asubuhi akafika Morogoro au Dodoma akafanya shughuli zake na kurudi Dar es Salaam siku hiyo hiyo.


Inachukua chini ya masaa manne kusafiri kwa treni ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma, wakati usabiri wa basi hutumia muda mrefu mara mbili ya huo.


Tanzania inatarajiwa kupata mapinduzi makubwa kwenye maendeleo yake kutokana na ujenzi wa reli ya SGR unaofanywa na Serikali ya Rais Samia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso