Na Suzy Butondo, Shinyanga press blog
Hatimaye mtoto mchanga wa jinsia ya kike aliyekuwa ameibiwa Agosti 20,2024 majira ya saa 12:00 jioni huko katika kijiji cha Mbika kwenye kituo cha afya Ushetu wilayani Kahama mkoa wa Shimyanga amepatikana.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Agosti 24,2024 ofisini kwake amesema mtoto huyo alikuwa amezaliwa Agosti 17,2024 na mama yake mzazi, ambapo aliendelea kuwepo kituo cha afya kwa uangalizi zaidi, baada ya mama mzazi kutoka nje kufanya mazoezi ndipo mtuhumiwa alimuiba mtoto huyo.
Magomi amesema taarifa za tukio hilo ziliripotiwa kituo cha polisi Nyamilangano mnamo Agosti 21, 2024 mara baada ya kupokelewa jeshi la polisi, lilipokea taarifa hizo na ufuatiliaji wa haraka ulifanyika, na agosti 22,2024 majira ya saa tatu usiku askari polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa aitwaye Hadija Juma (24) mkazi wa kijiji cha Sengerema Wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora akiwa na mtoto huyo.
Mtuhumiwa huyo amekamatwa na kuhojiwa na kukiri kutenda kosa, hivyo taratibu za kumfikisha mahakamani zinakamilishwa, na jeshi la polisi linaendelea kuwashukuru wananchi kwa kutoa taarifa za waharifu na uhalifu na wanahimizwa waendelee kufanya hivyo.
"Mtuhumiwa huyo baada ya kumhoji alisema amefanya uhalifu huo baada ya kuolewa mara mbili bila ya kufanikiwa kupata mtoto ambapo aliolewa ushetu miaka miwili hakupata mtoto akaolewa wilaya ya Uyui hakupata mtoto hivyo aliamua kufanya uharifu wa kuiba mtoto huyo,"amesema Magomi.
"Tunawashukuru sana wananchi waliweza kutupa taarifa kwamba mtuhumiwa huyo alikuwa akifika hospitalini hapo kwa ajili ya kusalimia wagonjwa na wazazi, lakini siku hiyo mzazi wa mtoto huyo alikuwa akifanya mazoezi, ndipo mama huyo alipata nafasi ya kumuiba mtoto huyo na kuondoka naye kwenda mpaka wilaya ya Uyui mkoani Tabora ambapo ndiko tumemkamatia,"ameongeza
Kamanda ametoa wito kwa wanawake wanaopata changamoto ya uzazi wakutane na wataalamu wa afya, ili waweze kusaidiwa zaidi waweze kupata watoto kuliko kukimbilia kuiba
No comments:
Post a Comment