Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu amesisitiza msimamo wake wa kutaka kujibiwa kwa hoja za aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa ambaye sasa amejiunga na CCM.
Sambamba na hilo, amesisitiza pia msimamo wake wa kuondoka ndani ya Chadema iwapo kitakwenda kinyume na sababu zilizomfanya ajiunge nacho akisema, “Chadema sio mama yangu.”
Kwa mara ya kwanza, Lissu alionyesha msimamo wa kutaka kujibiwa kwa tuhuma zinazoibuliwa na Mchungaji Msigwa dhidi ya Chadema tangu Juni mwaka huu alipowasili nchini akitokea Ubelgiji.
“Kwa kuzingatia tuhuma zenyewe, zinatakiwa zijibiwe. Kama mali zisizohamishika majengo na chochote kitakuwa na nyaraka, lakini kama mali zinazohamishika kama fedha hizo vile vile zina nyaraka,” alisema Lissu alipozungumza na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Miongoni mwa tuhuma zinazoibuliwa na Msigwa dhidi ya Chadema tangu alipohamia CCM, Juni 30 mwaka huu, ni ufisadi anaodai upo ndani ya chama hicho.
Moja ya matendo aliyoyarejea kama ya kifisadi ni fedha zaidi ya Sh2 bilioni walizochangishwa waliokuwa wabunge wa chama hicho mwaka 2015, ambazo amedai hadi sasa haijulikani zilipokwenda.
Lissu ameyasema hayo jana usiku Agosti 17, 2024 alipohojiwa katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Kituo cha Luninga cha Star TV.
No comments:
Post a Comment