Shinyanga waupiga mwingi miradi ya maendeleo mwenge wa uhuru
Na Marco Maduhu,TABORA
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Godfrey Mnzava, ameupongeza mkoa wa Shinyanga kwa kuwa na miradi mizuri ya maendeleo, ambayo imemulikwa na mwenge wa uhuru.
Amebainisha hayo leo Agosti 16,2024 wakati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, alipokuwa akiukabidhi Mwenge huo wa uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chaha, makabidhiano yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Igusule wilayani Nzega mkoani Tabora.
Amesema mwenge wa uhuru ulipokuwa ukikimbizwa mkoani Shinyanga umepitia,kukagua,kufungua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi, kwenye miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa mizuri.
"Shinyanga tumemeona miradi ya maendeleo na tumepata ushirikiano wa kutosha,kwa kweli mmeupiga mwingi kama Yanga," amesema Mnzava.
"Miradi yote ya maendeleo ambayo tumeizindua tunaomba itunzwe na kuendelea kuhudumia wananchi, na ile ambayo tumeweka mawe ya msingi ikamilishwe kwa wakati," ameongeza Mnzava.
Aidha,amewataka pia wananchi kwamba wazingatie kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu 2024, kwamba watunze mazingira pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, akizungumza wakati wa kukabidhi mwenge huo mkoani Tabora, amesema ukiwa mkoani humo umekimbizwa umbali wa kilomita 643.2 na kumulika miradi ya maendeleo 46 yenye thamani ya Sh.bilioni 26.4.
Amesema kwa miradi ya maendeleo ambayo imezinduliwa wataendelea kuitunza, na ile ambayo imewekewa mawe ya msingi wataisimamia na kuikamilisha kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Mwenge wa uhuru ulipokewa mkoani Shinyanga Agosti 10 mwaka huu ukitokea Mkoani Simiyu, na leo Agosti 16 umekabidhiwa mkoani Tabora.
Kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu inasema "Tunza mazingira na Shiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu".
No comments:
Post a Comment