JESHI LA MAGEREZA LIMEKABIDHI MADAWATI YENYE THAMANI YA SH MILIONI 20.8 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday 17 August 2024

JESHI LA MAGEREZA LIMEKABIDHI MADAWATI YENYE THAMANI YA SH MILIONI 20.8


JESHI la Magereza limekabidhi madawati, viti na meza vyenye thamani ya Sh. millioni 20.8 katika Shule ya Msingi Chinangali II, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni kusaidia kupunguza changamoto ya madawati shuleni hapo

Awali, dawati moja lilikuwa likikaliwa na wanafunzi watano jambo lililokuwa likisababisha adha kwa wanafunzi hao.


Jeshi hilo limekabidhi madawati 55, viti na meza zake ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Ramadhani Nyamka hivi karibuni.


Wakizungumza baada ya kukabidhiwa madawati  wanafunzi wa shule hiyo wamelishukuru jeshi hilo na kusema yameenda kutatua changamoto ya kubanana katika dawati moja darasani.



“Mwanzoni tulikuwa tunakaa kwa kubanana lakini sasa tutaweza kukaa darasani kwenye madawati kwa nafasi.” Alisema Alfred Daus, mwanafunzi wa darasa la saba.



Naye Pascal Joel mwanafunzi wa darasa la saba alisema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga miundombinu bora inayopelekea wanafunzi kupata elimu bora kwa sasa.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Tulinagwe Ngonile alisema kuwa madawati hayo yatawezesha wanafunzi 165 kukaa kwenye madawati na kwamba watasoma katika mazingira rafiki.


Akizungumza baada ya kukabidhi madawati hayo, Kaimu Kamishna wa Huduma za Urekebu Jeshi la Magereza, Bertha Minde alisema kuwa ujio wa madawati 55, viti na meza zake ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Ramadhani Nyamka mwaka jana wakati wa Mahafali ya darasa la saba shuleni hapo ambapo shule iliomba kupatiwa madawati na samani mbalimbali ahadi ambayo sasa imetekelezwa.


Imeandaliwa na Sifa Lubasi 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso