Na Elizabeth Zaya,Matukio Daima App
NAIBU Waziri Mkuu NAIBU Waziri Mkuu, Dk.Doto Biteko amewataka wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), kuwachagua viongozi wao wanaotaka kusukuma haki na amani ya Tanzania, watakaowaunganisha badala ya kuwagawanya na watakaokuwa na matamko ya kitaaluma.
Kadhalika, amewataka kuwachagua ambao wataiweka taaluma yao kuwa ya heshima kwa jamii na siyo kujitafutia wao umaarufu.
Dk.Biteko ametoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa TLS ambao pamoja na mambo mengine utachagua viongozi wa chama hicho akiwamo rais na makamu wake.
“Inawezekana namna anavyozunguma hakufurahishi, au anatokea mahali ambako wewe hautokei, lakini kama agenda yake ni kuufanya uwakili kuwa jambo la heshima kwenye jamii yetu na siyo yeye binafsi kuwa maarufu, huyo, mfikirieni, mahali penye kuvumiliana pana maendeleo,”amesema Dk.Biteko.
Amewataka watakaochaguliwa kufanya kazi ya kuwaunganisha na wale watakaoshindwa kuwaunga mkono watakaoshinda.
“Na hicho ndicho kinatufanya tuwe wanadamu, tofauti zetu, lakini uwapo wenu kuna kitu kimoja kinawaunganisha, chenyewe hakiangalii tofauti hizo, ambacho ni taaluma na uanasheria wenu, kama atatokea mtu anaumizwa zaidi na uwakili wenu na angetamani unakuwa na maana kwa jamii ya Watanzania kwa ajili ya kusukuma haki na amani, ningekuwa mpiga kura ningesema huyo mwangalieni,”amesema Dk.Biteko.
Ametoa wito kwa chama hicho, kuendelea kuwa na msisitizo wa kwa wanataaluma kukaa kwenye taaluma yao kama wanasheria na kuwa na kiu ya kuendeleza chama chao.
“Muendelee kuwa na kiu ya kuona chama chenu kinakuwa zaidi na kinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya Watanzania wote. Nataka niwape siri moja wakati mnachaguana. Haiwezekani ndugu rais ukawa na chama cha watu wote hawa wasiwe na kabila, dini, wasiwe na mapenzi na timu ya mpira.
“Wamo wa timu nyingine, na wengine wana timu hii, au wana vyama vya siasa au ukanda wanakotokea, wameumbwa na Mungu, mvumiliane,”amesema Dk.Biteko.
No comments:
Post a Comment