BEI YA UMEME TANZANIA NI NAFUU KULIKO NCHI NYINGINE ZA AFRIKA MASHARIKI-KAPINGA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 30 August 2024

BEI YA UMEME TANZANIA NI NAFUU KULIKO NCHI NYINGINE ZA AFRIKA MASHARIKI-KAPINGA

 





📌 *Ni kutokana na Serikali kuweka ruzuku katika kila uniti*


📌 *Aelezea ruzuku inayotolewa na Serikali kufikisha umeme visiwani*


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema gharama ya kununua umeme nchini ipo chini ukilinganisha na Nchi nyingine za Afrika Mashariki.


Hii ni kutokana na Serikali kuweka ruzuku kwenye gharama ya mwananchi kununua umeme.


Mhe. Kapinga amesema hayo leo Agosti 30, 2024 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu maswali ya Wabunge ambao walitaka kufahamu iwapo kuanza kwa uzalishaji umeme katika mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) kutapunguza gharama ya ununuzi wa umeme na lini Serikali itashusha bei ya umeme.


"Mheshimiwa Spika, bei ya sasa ya umeme tayari ina ruzuku za Serikali ndani yake ambapo kwa sasa wastani wa bei ya uniti 1 ya umeme yenye ruzuku ni shilingi 100 kwa matumizi ya kawaida chini ya uniti 75 kwa mwezi na bila ruzuku inakuwa shilingi 292." Amefafanua Kapinga.


Ameongeza kuwa, kwa mwananchi anayetumia zaidi ya uniti 75 kwa mwezi, analipa kiasi cha shilingi 292 kwa uniti 1 ya umeme yenye ruzuku badala ya shilingi 320 bila ruzuku.


Kuhusiana na suala la kupunguza bei ya uniti za umeme, Mhe. Kapinga amesema Serikali itaendelea kufanya tathmini ya gharama za utoaji wa huduma za TANESCO mara kwa mara na kuendelea kurekebisha bei kulingana na gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme utakavyokuwa.


Akijibu swali kuhusu mradi wa upelekaji wa umeme kwenye maeneo ya migodi iliyopo Chunya, mkoani Mbeya, Mhe. Kapinga amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi ili akamilishe mradi huo mapema.


Kuhusu ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Hanang mkoani Manyara amesema ujenzi wake utatekelezwa katika mradi wa gridi imara Awamu ya Pili.


Akizungumzia upelekaji umeme wa gridi kwenye maeneo ya Visiwa, Mhe. Kapinga amesema Tanzania ina visiwa takriban 120 na Serikali imeanza kufanya tathmini ya kufikisha umeme wa gridi katika maeneo hayo.


Ameongeza kuwa, kwa sasa visiwa hivyo vinatumia umeme wa jua ambapo Serika imeweka ruzuku ya asilimia 50 hadi 55 ili wananchi wapate umeme wa uhakika kwa muda wote.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso