WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUTUMIA FURSA YA SHEREHE ZA WAKULIMA, WAVUVI NA WAFUGAJI ‘NANENANE’ KUTANGAZA UTALII WA NDANI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 19 July 2024

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUTUMIA FURSA YA SHEREHE ZA WAKULIMA, WAVUVI NA WAFUGAJI ‘NANENANE’ KUTANGAZA UTALII WA NDANI



Na John Bera – Dodoma


Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kutumia fursa ya Sherehe za Wakulima, Wavuvi na Wafugaji zilizopangwa kufanyika Eneo la Nzuguni, Jijini Dodoma tarehe 01 hadi 08 Agosti, 2024 kutangaza utalii wa ndani kwa kuhamasisha uwekezaji na wananchi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Dodoma na maeneo ya karibu.


Akizungumza kwenye Kikao cha Maandalizi ya Maonesho hayo, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi kwa upande wa Wizara, Bw. Emmanuel Msoffe amesema Wizara imejipanga kuhakikisha inatangaza vivutio vya utalii vilivyopo maeneo mbalimbali nchini, kuhamasisha shughuli za uwekezaji kwenye sekta ya utalii, maliasili na malikale pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kutembelea maeneo ya vivutio vinavyosimamiwa na taasisi zake za Uhifadhi kwa utaratibu maalum.


Amesema ‘’Sherehe za Nanenane kwa mwaka huu zinazafanyika Jijini Dodoma ambapo zitafunguliwa na kufungwa na viongozi wakubwa wa kitaifa, hivyo, Wizara inaendelea kujipanga vizuri kushiriki kikamilifu katika kutangaza utalii hususan utalii wa ndani’’ .


Kwa kawaida, Wizara imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya utangazaji utalii ambapo maonesho na matukio (MICE) kama Sherehe za ‘Nanenane’ ni fursa muhimu katika utangazaji utalii. Jitihada hizo zinaenda sambamba na kuunga mkono azma ya Serikali ya kufikia idadi ya watalii milioni 5 na mapato yatokanayo na utalii Dola za Marekani bilioni 6.


Sherehe za Wakulima, Wavuvi, na Wafugaji hufanyika kila mwaka ambapo kitaifa hufanyika kwa mzunguko katika Kanda mbalimbali ambapo kwa mwaka huu, 2024, kitaifa zitafanyika Jijini Dodoma.


Sherehe hizo zinalenga kutambua mchango wa sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji katika ukuaji wa uchumi, kuwakutanisha wadau wa sekta husika kubadilishana uzoefu na kuonesha shughuli na fursa zilizopo kwenye sekta hizo. Mgeni Rasmi wakati wa kilele cha sherehe hizo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


Sekta za Maliasili na Utalii ni sekta muhimu zinazofungamanishwa kwenye sekta za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji ili kuimarisha mnyororo wake wa thamani. Hivyo, Wizara, taasisi chini ya Wizara na wadau wa sekta binafsi za utalii na maliasili wanatarajiwa kushiriki sherehe hizo






No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso