WACHIMBAJI FUATENI SHERIA ZA MADINI KUEPUKA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI-ENG KUMBURU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday 1 July 2024

WACHIMBAJI FUATENI SHERIA ZA MADINI KUEPUKA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI-ENG KUMBURU


Afisa madini mkazi Mkoa wa kimadini Kahama, Eng Joseph Kumburu, akizungumza wakati wa mafunzo juu ya utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa shughuli za madini, kodi na tozo mbalimbali za serikali, pamoja na wachimbaji kufuata taratibu sahihi za utoaji wa huduma kwa wateja ili kulinda maslahi mapana ya serikali kwenye suala la kudhibiti utoroshwaji wa madini ya dhahabu katika maeneo ya uchimbaji


NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL-KAHAMA


Mwenyekiti wa SHIREMA mkoa wa Shinyanga Hamza Tandiko akimuomba afisa madini kuwafafanulia kuhusu suala la kodi pamoja na tozo nyingi wanazolipa kwenye biashara ya madini



Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mkoa wa kimadini Kahama, wametakiwa kufuata sheria za madini ili kuepuka utoroshaji wa madini kwani kufanya hivyo ni kuhujumu Uchumi wa nchi.

Wito huo umetolewa na afisa madini mkazi mkoa wa kimadini Kahama, Eng Joseph Kumburu, wakati wa mafunzo juu ya utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa shughuli za madini, kodi na tozo mbalimbali za serikali, pamoja na wachimbaji kufuata taratibu sahihi za utoaji wa huduma kwa wateja ili kulinda maslahi mapana ya serikali kwenye suala la kudhibiti utoroshwaji wa madini ya dhahabu katika maeneo ya uchimbaji, yaliyofanyika katika eneo la Mgodi wa Nyamishiga Halmashauri ya Msalala.

Eng Kumburu amesema serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki kwa wachimbaji wadogo, lakini changamoto ya baadhi yao kutofuata sheria bado imeendelea kushuhudiwa katika maeneo ya mialo, suala ambalo ni kinyume cha utaratibu na sheria za madini, na kwamba ofisi yake imeona ni vyema kuwekeza kwenye elimu zaidi huku ufuatiliaji na hatua zaidi zikiendelea kuchukuliwa.

“Tumesema tusikamatane, tupeane elimu, tuelimishane taratibu zikoje tuwaambie taratibu zote za mialo, watoroshaji siku hizi wanapitia kwenye mialo huko huko, kwa sababu kwenye Elution tupo, migodi ya kati tupo serikali, mikubwa tupo, huku chini sasa kwa sababu nyie mko wengi sisi tuko wachache hatuwezi tukamsimamia kila mmoja kwenye eneo lake, ndio maana mialo inatakiwa iwe eneo moja iwe ni rahisi afisa wa madini au afisa wa serikali kwenda kusimamia” Alisema Eng Kumburu



“Lakini unakuta mwingine mwalo amepeleka nyumbani kwake, mwingine mara amepeleka karibu na bar, mwingine mwalo ameweka sehemu ya kuchimba, sasa tunawaomba wasimamizi muongeze usimamizi kwenye watu wa mialo kwa sababu utoroshaji unapita kule, kuna watu wanajiita makota, gharama za ile leseni ni laki mbili na nus utu, serikali imeweka masoko ya madini, imeweka huku kwenye maeneo ya wachimbaji, tena nyinyi mna bahati tumewawekea kituo tu hapa karibu, kama tumesogeza kituo hapa hapa kwenye uchimbaji, inakuwaje hapa panakuwa na utoroshaji? Makarasha yanazunguka kila siku mpaka saa 12 ila dhahabu haionekani, kama unasereresha basi Andika, ijulikane wewe utaratibu wako ni kusereresha, kama watu wanakuja kwako kuzalisha basi waandike, kama mtu hataki inamaana ni mtoroshaji, toa taarifa” Aliongeza Kumburu

Awali wakizungumza kwenye mkutano huo, mwenyekiti wa SHIREMA mkoa wa Shinyanga Hamza Tandiko alimuomba afisa madini kuwafafanulia kuhusu suala la kodi pamoja na tozo nyingi wanazolipa kwenye biashara ya madini, huku mwenyekiti wa akina mama wachimbaji Tanzania TAWOMA Semeni John, akieleza kutoridhishwa na namna wanavyouza madini lakini hawapewi stakabadhi kuonyesha kama kodi zao zimeingia serikalini ama laa.

Akizungumzia changamoto hiyo, Eng Kumburu amesema suala la tozo litafanyiwa kazi kwa kushirikiana na Halmashauri, huku akieleza kuwa sheria ya madini inamtambua mwenye leseni au aliyepewa jukumu la kusimamia eneo husika, ambaye anatakiwa kuchimba na wanachama wake au mtu aliyeingia nae ubia.

“Kwa hiyo ukipewa leseni iwe ndogo, kubwa au ya Katikati unatakiwa uchimbe wewe na wanachama wako au mlete m-bia kule ndani na ukichimba kwenye leseni haitakiwi kitu chochote kitoke nje ya leseni” Alisema Eng Kumburu

Shida ya sisi Watanzania tunaoneana huruma mwenye leseni au msimamizi analeta watu, mbaya zaidi inawezekana hata yeye hachimbi, ndio nyie wote mmekuja kuchimba hapa lakini mnasimamiwa na msimamizi wa eneo hili ama mwenye leseni, kwa hiyo mimi kama afisa madini natakiwa nimtambue niliyemkabidhi pale kwa sababu nikisema nimtambue mwenye duara akitoroka naenda kumpata wapi? Lakini mwenye leseni hawezi kukimbia maelezo yake yote ninayo. Aliongeza

“Sasa mwenye leseni au msimamizi anapowasimamia wale watu yeye ndo anapokea ile kodi kwa niaba ya wale wenzake analeta kwetu, ndio maana Waziri wa madini Mhe. Anthony Mavunde amekuja na kitu kinaitwa mkataba kati ya mwenye leseni na mwenye duara au msimamizi na mwenye duara maana yake mtambulike sasa, kwa sababu hata wenye mialo kupitia hivi vitabu wanatambulika sasa hata wakienda kulalamika sehemu ofisi ya madini inamtambua kwa sababu amesajiliwa, sasa zile tozo nyingi ndo zinaanzia hapa.” Alisema Eng Kumburu

Akizungumzia suala la stakabadhi amesema zinatolewa kwa mujibu wa sheria, na kuwataka kila anauza adai risiti kwa kufuata utaratibu na atapewa.


Mwenyekiti wa akina mama wachimbaji Tanzania TAWOMA Semeni John, akieleza kutoridhishwa na namna wanavyouza madini lakini hawapewi stakabadhi kuonyesha kama kodi zao zimeingia serikalini ama laa

baadhi ya wachimbaji wa wadogo wa mgodi wa Nyamishiga wakipata mafunzo

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso