Na WAF - Dar Es Salaam
Taasisi ya Benjamini Mkapa kwa kushirikiana na Serikali imejikita katika kutatua changamoto za rasilimali watu Sekta ya Afya kwa kuajiri watumishi wa mikataba na kuwapeleka Mikoa ya pembezoni mwa nchi ikiwemo Rukwa, Simanjiro, Katavi hali ambayo inasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi.
Baada ya Mikataba yao kuisha watumishi hao wa BMF huwa wanapewa ajira za kudumu na Serikali ambapo hupelekea kupatikaa kwa huduma za Afya kwa urahisi.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Julai 30, 2024 wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambae ni mgeni rasmi kwenye Kongamano la majadiliano ya Kitaifa kuhusu masuala ya rasilimali watu katika Sekta ya Afya linalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam.
"Kongamano hili ni sehemu ya kuuenzi mchango wa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa ambapo uongozi na maono yake ya kuboresha Sekta ya Afya yameacha alama kubwa nakuweka misingi ya mikakati ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na Afya njema." Amesema Waziri Ummy
Aidha, katika Kongamano hilo Waziri Ummy ametoa rai kwa Sekta binafsi pamoja na vyuo vya mafunzo vinavyotoa wataalamu wa Afya kuzalisha wanataalum wenye uwezo wa kutoa huduma bora za Afya ambazo ni bora na salama kwa wananchi.
"Hivi sasa tunazungumzia kuwapeleka nje ya nchi kwenda kutoa huduma za Afya, je wataalam tunaozalisha hapa nchini kwetu leo wanaweza kwenda kuajirika nchi za nje? Na wakafanya kazi vizuri kwa kuzingatia weledi wao." Amehoji Waziri Ummy
Waziri Ummy amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majali kwa kuwa mstari wa mbele kila linapokuja swala la Afya kwa kuwa muhamasisha mkubwa wa vijana katika kupima UKIMWI kujua hali, lakini pia kuwa muhamasishaji mkubwa wa watu kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa Yasiyoambukiza.
"Inasikitisha sana kuona takwimu za magonjwa ya Moyo, magonjwa ya Kisukari, Shinikizo la Juu la Damu yanazidi kuongezeka ili hali tunaweza kuyapunguza kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha na kuepuka tabia bwete." Amesema Waziri Ummy
Taasisi ya Benjamini Mkapa imeandaa Kongamano hili ikiwa ni sehemu ya kutambua, kuenzi na kumkumbuka aliyekuwa Rais wa awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamini Mkapa ambae alikua ni Mmoja wa vinara ambao walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za Afya ikiwemo Sheria ya Bima ya Afya ya (NHIF).
No comments:
Post a Comment