NIMEFURAHI KUONA SHULE YA WASICHANA MKOA WA KIGOMA IMEPOKEA WANAFUNZI – MHE. KATIMBA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 13 July 2024

NIMEFURAHI KUONA SHULE YA WASICHANA MKOA WA KIGOMA IMEPOKEA WANAFUNZI – MHE. KATIMBA




Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amesema, amefurahi kuona shule mpya ya maalum ya wasichana ya mkoa wa Kigoma imepokea wanafunzi kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mhe. Katimba ameshuhudia wanafunzi wakiwa katika shule hiyo maalum ya wasichana ya mkoa wa Kigoma, alipoitembelea kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha ujenzi wa shule hiyo ambayo imejengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.


Mhe. Katimba amesema, Rais Samia alitafuta fedha za kujenga shule maalum za sayansi za wasichana kila mkoa ili kuwawezesha kupata miundombinu bora itakayokuwa chachu kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi.


“Wanasayansi wetu wa kesho si mmeona jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha amewajengea shule nzuri hivyo jukumu lenu kubwa ni kuhakikisha mnasoma kwa bidii,” Mhe. Katimba amewaasa wanafunzi wa shule hiyo.


Mhe. Katimba amewataka wanafunzi hao kuzingatia masomo ili wamalize shule salama na baadae wawe na maisha bora yaliyochagizwa na miundombinu bora ya elimu ambayo imejengwa na Rais Samia ambaye tangu aingie madarakani alidhamiria kuwapatia fursa watoto wa kike ya kupata elimu bora.


“Msichanganye elimu na mambo mengine yatakayowakwamisha kutimiza ndoto zenu za kuwa wahandisi,madaktari, marubani na wanasayansi mnaotegemewa nchini na kwenye mataifa mengine,” Mhe. Katimba amewasisitiza.


Ujenzi wa shule hiyo utakamilika kwa asilimia 100 mara baada ya hivi karibuni Serikali kumalizia kupeleka fedha za awamu ya pili kiasi cha shilingi bilioni 1.1 ambapo hapo awali, ilipeleka kiasi cha shilingi bilioni 3 ambazo zimetumika kujenga miundombinu bora iliyopo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso