Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Andrea Mathew amekagua kazi za ujenzi wa upanuzi wa mradi wa maji kutoka line ya Mhangu-Ilogi kwenda Nyijundu, Bululu, Ifugandi na Busolwa katika Wilaya Nyang'hwale Mkoani Geita na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili ifikapo Agosti 17 mwaka huu wananchi wa maeneo husika wapewe huduma ya maji safi na salama.
Mhandisi Kundo Mathew amesema hayo leo tarehe 19 Julai 2024 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Nyang'hwale ambapo amesema wananchi wanashauku kubwa na upatikanaji wa maji safi na salama.
Naibu Waziri Kundo Mathew amesema ameridhishwa na maendeleo ya upanuzi wa mradi kutoka line ya Mhangu-Ilogi (JWPP) kwenda katika maeneo ya Wilaya ya Nyang'hwale.
Katika hatu nyingine amemtaka Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyang'hwale Mhandisi Moses Mwampunga kuhakikisha vijiji 15 ambavyo havijafikiwa na miradi ya maji vinafikiwa kwa haraka kwa kutumia uchumbaji wa visima. Wilaya ya Nyang'hwale ina jumla ya vijiji 62 na mpaka sasa vijiji 47 vimekwishafikiwa na huduma ya maji. Pia akisisitiza maeneo yatakayotembelewa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu yawe na huduma ya maji kwa wananchi.
"Hatutaki kwenda kwenye uchaguzi vijiji vya hapa Nyang'hwale vikiwa havina huduma ya maji hakikisheni hili mnalisimamia kwa nguvu zote"
"Lengo ni kwamba Mwenge wa Uhuru unapokuja kukagua unaangaza miradi inayotekelezwa lakini kwa ubora wake na thamani ya pesa katika miradi hiyo"
"Kwahiyo tuhakikishe miradi yetu yote inakaa vizuri, sisi sekta ya maji mwaka huu kwa maelekezo ya Waziri wetu Juma Aweso tunataka katika miradi ambayo inakaguliwa na Mwenge wa Uhuru ikaongoze Kitaifa hiyo ndiyo dira ya Waziri wetu''amesisitiza Naibu Waziri wa Maji Kundo Mathew.
Aidha amesisitiza katika utunzaji wa vyanzo vya maji, ulinzi wa miundombinu pamoja na kushiriki katika uchangiaji wa kipato kidogo ambacho kitawezesha miradi kuwa endelevu.
Akipokea maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita Mhandisi Jabiri Kayilla ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo na kufikia tarehe 17 mwezi Agosti wananchi watakuwa wameanza kupata huduma katika mradi wa Nyijundu na mradi wa Bululu/Ifugandi/Busolwa wenyewe umeshaanza kutoa huduma.
Akisoma taarifa ya upanuzi wa mradi wa maji kutoka line ya Mhangu-Ilogi kwenda Nyijundu, Bululu, Ifugandi na Busolwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyang'hwale Mhandisi Moses Mwampunga amesema katika kipindi cha miaka mitatu (03) kuanzia 2022 hadi 2024 miradi ya maji mikubwa saba (7) imetekelezwa kufanya ongezeko la maji kutoka asilimia 39 hadi 75.
No comments:
Post a Comment