Na Anangisye Mwateba-Hifadhi ya Taifa Ruaha-Iringa
The Great Ruaha Marathon zitaendelea kukimbiwa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kwani mbio ambazo zinatangaza utalii moja kwa moja kutokea kwenye moja ya vivutio vya utalii vinavyopatikana nyanda za juu kusini.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa(Mb) alipokuwa akitoa hotuba kwa washiriki wa Mbio za Great Ruaha Marathon ambazo zimefanyika katika Hifadhi ya Ruaha Mkoani Iringa.
Aidha Mhe. Waziri Mkuu pamoja na kusisitiza juu ya masuala ya Utalii alisisitiza watanzania kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukizwa ikiwa ni pamoja na kula milo iliyokamilika kwa ajili ya afya yetu.
Mhe. Majaliwa aliendelea kueleza kuwa moja ya faida ya mbio za Ruaha ni kuonyesha mazuri ya uhifadhi wa maliasili zinazopatikana nyanda za juu kusini ikiwemo Hifadhi ya Taifa Kitulo na pori la akiba Mpanga kipengele.
Vilevile Mhe. Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kufanya uwekezaji kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa Ruaha, kwani kwa sasa Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuboresha miundo mbinu ikiwemo kujenga viwanja vya ndege ndani ya hifadhi na kuimarisha barabara za ndani ya hifadhi.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(MB) alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi anazoendelea kufanya ili kuboresha utalii nchini. Kupitia juhudi za Mheshimiwa Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii ilipata fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 150 ili kutekeleza mradi wenye lengo la kufungua utalii kusini mwa Tanzania.
Hifadhi ya Taifa Ruaha ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huu, ambapo ujenzi wa viwanja viwili vya ndege vyenye thamani ya Sh. 42,109,902,122.14 unaendelea. Sambamba na hilo, majengo yenye thamani ya Sh. 17,500,373,790.06 yanajengwa kwa ajili ya watumishi na malazi kwa wageni.
Pia, kupitia mradi huu Hifadhi iliweza kununua mitambo na malori 27, pamoja na magari madogo 11. Mradi huu pia unatoa ufadhili wa masomo kwa jamii jirani ambapo jumla ya vijiji 16 kutoka katika wilaya za Chamwino, Iringa na Mbarali vimenufaika.
No comments:
Post a Comment