Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kusoma kwa bidii ili taifa lipate viongozi bora wa baadae.
Wito huo ameutoa wilayani Uvinza wakati akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.
“Ndugu zangu hili ninalisema kutoka moyoni, hawa watoto hakikisheni wanakwenda shule na mfuatilie kama wanaenda kusoma na si kucheza, na msipowafuatilia hatutopata viongozi bora wa baadae watakaoendana na teknolojia ya kidijitali,” Mhe. Dkt. Mpango amesisitiza.
Dkt. Mpango amesema, hatuwezi kupata madaktari bingwa na wataalam wa kada nyingine kama watoto hawajasoma vizuri na kupata elimu itakayowawezesha kuwa wabobevu katika fani mbalimbali.
“Tunataka madaktari, waalimu, wahandisi na viongozi wa ngazi zote ambao watakuwa wemesoma vizuri, hivyo wasimamieni watoto wasome kwa bidii kwani tusipowekeza kwenye elimu tutaendelea kusuasua,” Mhe. Dkt. Mpango amehimiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amewataka wazazi nchini kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha watoto wanakwenda shule na wanapata elimu bora itakayokuwa na manufaa na tija kwa taifa.
“Wazazi jukumu letu kubwa ni kuhakikisha watoto wanakwenda shule, kwani Serikali ya Awamu ya Sita imetumia fedha nyingi kujenga miundombinu bora ya shule za awali, msingi na sekondari ili watoto wa kitanzania wapate elimu bora,” Mhe. Katimba amesisitiza.
Mhe. Katimba ameanisha kuwa, katika mkoa wa Kigoma pekee Serikali imeleta bilioni 82 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu ampazo zimetumika kujenga miundombinu bora na rafiki inayowawezesha watoto kusoma.
No comments:
Post a Comment