MADIWANI FANYENI KAZI KWA WELEDI ILI MUACHE ALAMA - RC MACHA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 27 June 2024

MADIWANI FANYENI KAZI KWA WELEDI ILI MUACHE ALAMA - RC MACHA


RC Macha akiwataka watumishi na madiwani kuwa weledi katika kazi zao


NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL- MSALALA KAHAMA


MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka Watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Msalala kuwatumikia wananchi kwa weledi ili kuacha alama ya uwepo wao madarakani.


Mhe. RC Macha ameyasema haya Juni 26, 2024 kwenye Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Halmaahauri ya Msalala kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo ameipongeza Msalala kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu (3) mfululizo.


"Niwatake sasa Waheshimiwa Madiwani mfanye kazi kwa weledi zaidi katika kuwatumikia wananchi ili muache alama nzuri zenye tija na maslahi mapama ya wananchi pale ambapo mtakuwa mmeondoka madarakani, nanyi watumishi muishi kwa matendo na kufanya kazi kwa maadili safi kama hati mlizopata kwa miaka yote mitatu," amesema RC Macha.


Pia ameongeza kwamba Madiwani, watumishi na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaojenga barabara ya Kahama Kakola Km 74 kwa kiwango cha lami na kuweka ulinzi wa mali za wakandarasi wakati wote wa mradi.


Akiwasilisha taarifa hiyo Mhasibu wa Halmashauri ya Msalala Rumoka E Buholela amesema hoja 56 zilizoibuliwa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG, Kati ya hoja hizo 16 zimefungwa na hoja 34 ziko katika hatua za utekelezaji.


Kwa upande wake Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Shinyanga CPA. Yusuph Moeka amewashauri madiwani wa Msalala kuhakikisha wanaongeza jitihada katika kukusanya mapato ya Serikali, kuepuka matumizi ya fedha mbichi na badala yake makusanyo yote yanayofanywa yapelekwe Benki kwa wakati .


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) amewakumbusha watumishi wanaopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuleta tija katika kazi zao.


Katibu tawala wa Wilaya ya Kahama kushoto pamoja na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) wakisikiliza taarifa ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali

Madiwani wa halmashauri wakifuatilia kwa makini taarifa za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali


DC Mtatiro akiwakumbusha madiwani na watunishi kutumia dhamana zao za utumishi kuleta tija kwa wananchi

PICHA ZAIDI





No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso