FURSA YA ELIMU YA FEDHA YAWAFIKIA WANANCHI SHINYANGA. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday 25 June 2024

FURSA YA ELIMU YA FEDHA YAWAFIKIA WANANCHI SHINYANGA.



Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, wamepata fursa ya kujifunza elimu ya fedha kuhusu uwekezaji, matumizi sahihi ya fedha binafsi, utunzaji wa fedha binafsi, mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mikopo, faida ya kuwekeza kwa ajili ya maisha ya uzeeni na kustaafu ili kufanya maamuzi sahihi wanapotumia huduma za fedha na kukuza uchumi.


Akizungumza kuhusu maeneo yatakayofikiwa katika mkoa wa Shinyanga, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kupata elimu ya fedha kutokana na umuhimu wa elimu hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla.


‘’Wizara ya Fedha inaendelea na kutoa elimu ya fedha, na kwa sasa tupo katika Mkoa wa Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, baada ya hapa tutaelekea katika Wilaya nyingine za Msalala, Ushetu pamoja na Kahama, hivyo tunatoa wito kwa wananchi maeneo ambayo tutapita wajitokeze kwa wingi’’ Alisema Bi. Mnzava


Awali, kabla ya mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Anamringi Macha, aliwataka wananchi wa Mkoa wake kushiriki vyema katika mafunzo hayo kutokana na wananchi wengi mkoani humo kujihusisha na mikopo bila kuzingatia malengo hali inayosababisha kupata migogoro ya kifamilia mpaka kupoteza mali zao.


“Jamani! Watu wanaandikishwa kwenye mikopo bila mpangilio, utasikia niandikishe hata kabla hajajua mkopo una riba kiasi gani, akisikia tu kuna gari inatoa mikopo hapa kabla hajafika anapiga simu niandikishe anachukua mkopo bila malengo kwahiyo watumie elimu hii kama fursa’’ alisisitiza Bw. Macha.


Kwa upande wake Bi. Anastazia Elias mmoja wa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga aliyeshiriki mafunzo ya elimu ya fedha, alisema elimu ya fedha kwake ni jambo geni na anaipongeza Wizara ya Fedha kwa kumfungua macho katika suala zima la kuweka akiba na matumizi ya fedha kwa ujumla huku akiomba zoezi hilo liwe endelevu.


“Mimi kwanza sijawahi kuona lakini nimeona leo, elimu ya fedha imenipa mwanga mkubwa sana, maana maisha yetu tulikuwa tunayaendesha kibubu, hii huduma iendelee kutolewa zaidi maana sisi wanawake unakopa laki moja unafika nyumbani alfu thalathini yote imeisha kabla ya malengo uliyokopea’’ alisema Bi. Anastazia.


Naye Buhohela Shija, alisema kuwa kabla ya mafunzo hayo wananchi wengi hawakuwa na uelewa kwenye masuala ya fedha hivyo elimu hiyo ni vyema ikaendelea kutolewa kwa wananchi wote.


“Natoa shukrani zangu za dhati kwa ugeni huu wa Wizara ya Fedha kuja kutuletea elimu stahiki tumejifunza vya kutosha kuhusu uwekaji akiba maana watu wengi hatuna hiyo elimu’’ Alisema Bw. Shija


Wizara ya Fedha itaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Mikoa yote nchini kwa kuwa ni moja ya mpango wake wa kuhakikisha wananchi wote wanapata uelewa kuhusu huduma za kifedha ikiwemo masuala ya akiba, mikopo na uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso