BOT NA STAMICO WATOA SEMINA KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 13 June 2024

BOT NA STAMICO WATOA SEMINA KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KAHAMA







Meneja idara ya huduma za wakala wa serikali kutoka Benki kuu ya Tanzania BOT Sadiki Nyanzowa akizungumza na wachimbaji wadogo na wa kati katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama

NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL- KAHAMA

Serikali kupitia benki kuu ya Tanzania BOT, shirika la madini la Taifa – STAMICO, wizara ya fedha, wizara ya madini kupitia tume yake, ina mkakati wa kununua dhahabu ikiwa ni kuendana na mkakati wa BOT kutaka kuanzisha hazina ya dhahabu, ili iweze kuongeza hazina ya dhahabu itakayosaidia kuwa na dhamana ya kupata mikopo kutoka mataifa ya nje.

Hayo yamebainishwa na meneja idara ya huduma za wakala wa serikali kutoka Benki kuu ya Tanzania BOT Sadiki Nyanzowa, wakati wa semina ya BOT kuhusu dhamana za mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

“Benki kuu inataka kurejesha utaratibu wa kununua dhahabu ili iweze kuwa na hazina ya dhahabu, kwanini benki kuu inataka kufanya hivyo, inataka kufanya hivyo ili iweze kuongeza hazina yetu ya dhahabu ili iweze kusaidia tunapotaka kukopa huko nje tuwe na dhamana ambayo ni dhahabu” Alisema Nyanzowa

“La pili ambalo ni la msingi kabisa, benki kuu kama msimamizi wa hazina ya Taifa, inatunza akiba yetu kwa maana ya fedha za kigeni, kwa hiyo basi benki kuu inasimamia uhifadhi wa fedha za kigeni ambazo nchi inakuwa imepata” Aliongeza Nyanzowa

Alisema kutokana na jitihada hizo mbili na kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, BOT imeleta huduma/elimu juu ya dhamana ya mikopo kutokana na wachimbaji wa dhahabu kukabiliwa na changamoto ya mitaji kutokana na kutokukopesheka katika taasisi za kifedha kutokana na kuwa na dhamana zisizotambulika.

“Kwa nini wanakosa mitaji, kwa sababu hawakopesheki either wanaweza kuwa na dhamana ambazo hazitambuliki, au wanaweza kuwa hawana dhamana kabisa, au wanaweza kuwa na sababu nyingine ambazo mabenki yanaweza kuwa yamewapa taratibu lakini wanashindwa kutekeleza” Alisema Nyanzowa

“Sasa kwa kuliona hilo serikali ilianzisha mifuko hii muda mrefu mwaka 2005 mpaka 2018 ikasimama kwa sababu serikali ilikuwa ikijaribu kuweka utaratibu mzuri na miongozo bora ili iweze kuchagiza maendeleo ya nchi na hatimaye mwaka jana mwezi Septemba ikarudishwa tena na inasimamiwa na benki kuu kwa niaba ya serikali na inasimamiwa na upatikanaji wa dhamana kupitia mifuko hii inapatikana kwenye mabenki” Alieleza Nyanzowa

Akizungumza katika semina hiyo mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoani Shinyanga Hamza Tandiko aliisisitiza BOT kuharakisha mchakato wa mikopo hiyo na kuahidi kuwa wachimbaji wadogo wapo tayari kuwa waaminifu katika fedha itakayotolewa na serikali.

“Tuko tayari na tutakuwa tayari kuwa waaminifu wakati wowote kwa fedha itakayotolewa na serikali, kwa sababu dhamira yetu ni kuwa mabilionea wakubwa, niwaombe msirefushe mambo, nendeni mkaweke utaratibu mzuri, ambao utatufikia sisi kwa Nyanja zote” Alisema Tandiko

Nao wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu waliohudhuria semina hiyo, wakaitaka serikali kupitia wizara ya madini, kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kuwapimia maeneo ya leseni zao, ili kujua kama kuna madini ama laa, badala ya kukimbilia kuwapa mikopo ambayo baadae wanaishia kupata hasara.

Wakizungumza kwa niaba ya wachimbaji wenzao, wachimbaji Fadhili Kipindula na Nsajigwa Mwaipopo, walisema wanachohitaji kwa sasa ni kuhakikishiwa endapo maeneo yanayomiliki leseni yana madini ndipo wakakope.

“Stamico aje afanye utafiti kwenye yale maeneo, inawezekana tuna leseni 100 kumbe hayana kitu ni makaratasi kwa hiyo wakitufanyia utafita kwenye yale maeneo tukapata uhakika, ina maana sasa serikali itakuwa imeamua kwelikweli kuikomboa nchi Pamoja na wananchi wake ambao wako kwenye wimbi kubwa la umasikini” Alisema Kipindula

“Tulikuwa tunahitaji BOT kwa sababu nyie ndio mnaotoa policy kwenye hizi taasisi za kifedha, mnekuja na draft/ mpango wa kuzieleza hizi taasisi namna zinaweza zikawakopesha wachimbaji wadogo, maana hizi benki hazitaki kutukopesha” Alisema Mwaipopo

Mjiolojia kutoka shirika la madini la Taifa – STAMICO Denis Silas alieleza kuwa wizara imekuja na mkakati wa madini ni Maisha na utajiri 2030, kuhakikisha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia katika maeneo ya wachimbaji wadogo ambapo hadi sasa nchini Tanzania ni 16% tuya maeneo yamefanyiwa utafiti.

“Hadi sasa kwa nchi yetu ni 16% tu imefanyiwa utafiti, lakini kwa vision hii ni kwamba mpaka kufika 2030, 50% ya maeneo ya Tanzania yawe yamefanyiwa utafiti” Alisema Silas

Awali akifungua semina hiyo, mgeni rasmi katika semina hiyo mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita, alikiri kupokea malalamiko ya changamoto za ukopeshwaji kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Kahama.

“Changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiletwa kwangu moja kwa moja ni swala la ukopeshwaji kwenye sekta ya madini, tumejionea ni kwa namna gani ambavyo mazingira rafiki yamewekwa kwa ajili ya kuweza kuinua wachimbaji wadogo, wa kati laiki pia kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wa juu, wakati huo huo pia kupata uwekezaji kutoka nchi za nje na kuongeza tija ya wawekezaji wan je ambayo inakwenda na kuinua wawekezaji katika sekta ya madini ambao ni wazawa” Alisema Mhita
 Mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita akizungumza katika semina

Mjiolojia kutoka shirika la madini la Taifa – STAMICO Denis Silas akizungumza katika semina hiyo


Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoani Shinyanga Hamza Tandiko akiisisitiza BOT kuharakisha mchakato wa mikopo hiyo

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso