wananchi wanaodai hawajalipwa fidia kupisha mradi wa bomba la mafuta
NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL- KAHAMA
Baadhi ya Wananchi Katika eneo la Kimkakati la Viwanda la Dodoma Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga wameilalamikia serikali ya manispaa hiyo kwa kutokupewa fidia kutokana na maeneo yao kupitiwa na mradi wa bomba la mafuta
Eliainaswe Elibariki ameeleza kuwa maeneo hayo walipewa na serikali kwa lengo la kuyaendeleza na baada ya mradi wa bomba la mafuta ghafi kupita katika eneo hilo walitakiwa kupisha mradi na kufidiwa juu ya maeneo hayo ila mpaka sasa hawajapewa fidia.
"Eneo hili tulipewa na halmashauri mwaka 2016 kwa lengo la kuliendeleza na tumeliendeleza kwa kuweka misingi na kujenga nyumba, mwaka 2023 tuligundua kuwa eneo hilo limepitiwa na bomba la mafuta baada ya kuona bikoni kwenye maeneo yetu", alisema Eliainaswe
Pia Christina Kasumbai amesema kuwa baada ya kugundua kuwa eneo lake limepitiwa na mradi wa bomba la mafuta aliwatafuta wanaohusika na mradi huo kujua taratibu za kufuata ili waweze kulipwa fidia.
"Niliwatafuta watu wa bomba la mafuta kujua taratibu za kulipwa fidia ila sikupata majibu ya kurizisha, tukaamua kwenda Halmashauri kwa Mkuu wa Wilaya ambapo alituambia kuwa eneo hilo limelipwa Halmashauri",alisema Christina
Kwa upande wake Afisa mawasiliano wa bomba la mafuta (EACOP) Abbas Ibrahim amesema kuwa eneo linalolalamikiwa linamilikiwa na Manispaa ya Kahama kwa hiyo wamelipwa Manispaa kama waguswa wa mradi.
Hata hivyo Katibu tawala wa Wilaya Kahama Hamad Mbega ameeleza kuwa wao kama serikali wamechukua hatua kufatilia ukweli wa madai hayo na kugundua kuwa eneo hilo tayari limelipwa fidia hivyo wameamua kukaa na ofisi ya Mkurugenzi kujua namna gani wanaweza kutatua chamgamoto hiyo.
No comments:
Post a Comment