Serikali imesema haitawavumilia waajiri wote wa sekta binafsi ambao wanakata michango ya wafanyakazi wao bila kuiwasilisha katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwani hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria na linawanyima haki wafanyakazi ambao wanashindwa kulipwa mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za NSSF,
Jijini
Dar es Salaam.
Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Mhe. Ndejembi amewataka waajiri wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani watakaobainika hawatabaki salama na kuwa kumkata mfanyakazi fedha bila ya kuiwasilisha katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kunamletea usumbufu anapostaafu au ajira yake inapofikia ukomo kwa kushindwa kulipwa madai yao mbalimbali kwa wakati.
Amesema baadhi ya waajiri wanawasilisha kwenye Mifuko asilimia kumi ya mwajiriwa tu, lakini ule mchango wake wa asilimia kumi hauwasilishwi jambo ambalo ni kinyume cha sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo inamtaka mwajiri kumkata mfanyakazi asilimia zote ishirini ambayo ni ya kisheria
Mhe. Ndejembi amesema baadhi ya kero za wastaafu hususani za kusubiria mafao yao kwa muda mrefu
zinasababishwa na waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati
hivyo kupelekea adha kubwa kwa wastaafu na kudhani Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
ndio inayowazungusha jambo ambalo muda mwingine sio kweli.
“Sasa tutakuwa wakali sana kwa waajiri wote ambao hawajawasilishi
michango kwa wakati kwani suala hilo ni kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha
Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii kuhakikisha kuwa waajiri wanawasilisha michango
yao kwa wakati na hivyo tutasimamia jambo hili kwa ukali,” Amesema Mhe.
Ndejembi.
Mhe. Ndejembi ameridhishwa na namna ambavyo NSSF imekuwa ikifanya vizuri ambapo ukuaji wa Mfuko umekua zaidi kuanzia kipindi ambacho Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwezi Machi 2021, thamani ya NSSF ilikuwa trilioni 4.8 lakini ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita thamani imefikia trilioni 8.1.
“Huo ni ukuaji wa hali ya juu na hii inaonesha mafanikio makubwa
ya Serikali ya awamu ya sita na mafanikio ya utendaji mzuri ya Mfuko
inayofanywa na Bodi ya Wadhamini, Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa NSSF,” Amesema
Mhe. Ndejembi.
Amesema pamoja na mafanikio hayo lakini kuna mambo ya msingi tunataka tuyaone yakitokea ikiwemo kuongeza nguvu ya huduma kwa mteja ambaye ni Mtanzania anayechangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwa anahudumiwa kwa wakati na changamoto zao zinaendelea kupokelewa na kufanyiwa kazi.
Hata hivyo amesema NSSF katika kuendelea kuboresha huduma zake
imejenga mifumo ya TEHAMA katika kuhakikisha mwanachama anapata huduma kwa
haraka zaidi.
Kuhusu uwekezaji, Mhe. Ndejembi amesema fedha za Watanzania
ambazo zipo kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii atahakikisha zinawekezwa vizuri
na kwa uadilifu kwenye miradi itakayoleta matokeo chanya na kurejesha fedha za
wanachama ili kulipa mafao kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu, Bw. Mshomba amemshukuru Waziri kwa kufanya
ziara ya kikazi na kumuahidi kuwa yote aliyoelekeza na kuyawekea msisitizo
watahakikisha wanayatekeleza.
Bw. Mshomba amesema NSSF inaendelea kuweka mkazo katika
uboreshaji wa huduma kwa wateja na jambo hilo lipo katika Mpango Mkakati wa
Mfuko, ambapo kwa sasa wameelekeza nguvu kwenye matumizi ya TEHAMA.
Amesema wataendelea kufanya uwekezaji wenye tija kwa kufuata
miongozo ya Bodi ya Wadhamini, Benki Kuu ya Tanzania na Ofisi ya Waziri Mkuu na
amewaahidi wanachama kuwa dhamira ya NSSF ni kuhakikisha inakua kadiri ambavyo
matarajio ya Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuwafikia wanachama kutoka sekta binafsi
na sekta isiyo rasmi.
No comments:
Post a Comment