JUMLA ya wanafunzi 188,787 waliokidhi vigezo wakiwemo wenye mahitaji maalum 812, wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na vyuo vya kati kwenye fani mbalimbali katika mwaka wa masomo 2024/25.
Hayo yamesemwa leo Mei 30,2024 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na vyuo vya kati vya ufundi.
Mhe. Mchengerwa amesema serikali ya Awamu ya Sita, inayosimamiwa na Rais Samia Suluhu Hassan imehakikisha wanafunzi wote wenye sifa wamepata nafasi kwenye shule na vyuo vya elimu ya ufundi.
Amesema kuwa kati ya wanafunzi hao walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu 131,986 wakiwemo wasichana 66,432 na wavulana 65,554 wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kidato cha tano 622 zikiwemo mpya 82 zinazoanza mwaka huu wa 2024.
“Wanafunzi hao wamepangiwa shule katika mchanganuo ufuatao wanafunzi 1,462 wakiwemo wasichana 669 na wavulana 793 walipangwa katika shule za sekondari nane zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi ambazo ni Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri,Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls”amesema Mhe. Mchengerwa
Pia, amesema kuwa wanafunzi 6,576 wakiwemo wasichana 3,449 na wavulana 3,127 wamepangwa katika shule za sekondari za kutwa za kidato cha tano.
“Wanafunzi 123,948 wakiwemo wasichana 62,636 na wavulana 61,312 wamepangiwa katika shule za sekondari za bweni za kitaifa za kidato cha tano”amesema
Aidha amesema kuwa wanafunzi 56,801 wakiwemo wasichana 17,332 na wavulana 39,469 wamepangiwa kujiunga kwenye kozi na fani mbalimbali za Stashahada katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
“Mchanganuo wa wanafunzi hao ni 2,107 wakiwemo wasichana 804 na wavulana 1,303 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya Elimu ya Ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Usimamizi na Maendeleo ya Maji (WDMI).”amesema
Amesema wanafunzi wengine 2,019 wakiwemo wasichana 1,011 na wavulana 1,008 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya afya ngazi ya Stashahada.
Pia, wanafunzi 52,675 wakiwemo wasichana 15,717 na wavulana 37,158 wamechaguliwa kujiunga kwenye kozi mbalimbali zikiwemo za Kilimo, Ufugaji, Utawala, Biashara na zinginezo za Stashahada katika vyuo vya elimu ya ufundi mbalimbali nchini.
Aidha,amesema kuwa muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano utaanza Julai Mosi 2024, hvyo wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na masomo wanapaswa kuanza kuripoti shuleni kuanzia Juni, 30 mwaka huu na siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa 14 Julai 14.
Hata hivyo Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano katika kila Tarafa inatekelezwa, ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Sita.
“Upanuzi na ujenzi wa Shule Mpya za Kidato cha Tano na Sita uendelee kufanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza tahasusi za masomo ya Sayansi, Mikoa ihakikishe inakuwa na tahasusi zote za msingi katika shule zake ili kuwapunguzia wazazi/walezi na wanafunzi gharama za usafiri kwenda shule za mbali”,ameeleza
No comments:
Post a Comment