MHANDISI TUMAINI CHONYA MENEJA TANESCO KAHAMA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
NA NEEMA NKUMBI HUHESO FM&HUHESO DIGITAL- KAHAMA
Shirika la ugavi wa umeme Tanzania – TANESCO wilayani Kahama mkoani Shinyanga, limeombwa kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika eneo la viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mpunga katika kata ya Kagongwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo akiwemo Kisandu Peja, wametoa kilio chao mbele ya waandishi wa habari waliotembelea katika eneo hilo, na kwamba, hali ya upatikanaji wa umeme katika viwanda vyao bado ni ya kusuasua kwani wakati mwingine unakuwa hautoshelezi.
Mwanamke mjasiriamali anayeuza chenga za mchele katika eneo la mashine za Kagongwa Mwasi Njile, ameiomba serikali kuangalia upya changamoto ya umeme kwao ili waweze kuhudumia familia zao.
“Sisi wakina mama wajasiriamali tunaenda huku unapata kilo tano, unapata kilo kumi, lakini sasa tatizo ikiwa umeme hakuna unashindwa namna ya kufanya, ulishe nini Watoto na wakati sisi tukiwa tunazunguka hivi ndo tunapata chakula cha Watoto, tunaomba tu kama kuna uwezekano, watuboreshee miundombinu ya umeme” Alisema Mwasi Njile
Mfanyabiashara mwingine Malando Dila, amesema wamewahi kutoa kilio chao kwa aliyekuwa waziri wa nishati January Makamba, na wakaahidiwa kupatiwa Transfoma 10, lakini mpaka leo hawajatekelezewa ombi lao licha ya eneo hilo kuwa na wawekezaji wengi.
“Umeme kwa kweli ni changamoto, tuliomba tupatiwe Transfoma 10 au 8, na akaahidi kwamba zile Transfoma ataleta lakini mpaka leo Transfoma ni moja tu tuliyopata, uhitaji wa watu ni mkubwa na watu wameendelea kuwekeza kwa wingi tu eneo hili la Kagongwa” Alisema Dila
Mhandisi Tumaini Chonya, meneja wa TANESCO wilayani Kahama, amesema eneo la Kagongwa halina changamoto kubwa ya umeme, bali kilichopo ni uhitaji wa maboresho madogo kwenye viwanda vipya 10 vilivyofunguliwa hivi karibuni, ambavyo wameanza kuvishughulikia.
“Kagongwa pale tumeweka TRANSFOMA 8 za 500KVA, Transfoma ya 315 iko moja tu hizi ni kubwa sana, kwa hiyo viwanda vya Kagongwa si kwamba ni vingi vimezidi TRANSFOMA hapana, TRANSFOMA zipo za kutosha kuwahudumia wananchi wa Kagongwa” Alisema Chonya
“Watusikilize wataalamu tunawaambia nini na ushauri wetu wauzingatie, kukiwa kuna jambo lolote tunawaambia hapa msifanye hivi fanya hivi, sisi ndo wataalamu ambao tunawahudumia wao” Aliongeza meneja Chonya
Wilaya ya Kahama yenye Halmashauri tatu za Kahama Manispaa, Ushetu na Msalala, katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2024/2025, imetengewa kiasi cha shilingi Bilioni moja, kwa ajili ya miradi mipya ya umeme, huku eneo la viwanda Kagongwa likiwa limetengewa Zaidi ya shilingi milioni 315, kwa ajili ya uboreshaji wa umeme sambamba na utekelezaji wa miradi mipya vikiwemo viwanda vipya vitakavyoongezeka.
No comments:
Post a Comment