Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imepitisha Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024 na Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2024 ikiwa ni hatua muhimu katika kuzitafsiri sheria zilizotungwa na Bunge hivi karibuni.
Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazohusu uchaguzi ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024.
Kanuni hizo zilizopitishwa leo tarehe 11 Mei, 2024 kwenye kikao cha Tume kilichofanyika Mjini Unguja, Zanzibar pia zinatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ikiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Baada ya kupitishwa kwa kanuni hizo, hatua inayofuata ni kuzichapisha kwenye gazeti la serikali ili ziweze kutumika rasmi ambapo kwa mujibu wa Tume, Kanuni hizo zitachapishwa tarehe 17 Mei, 2024.
Kanuni hizo zimepitishwa baada ya kuandaliwa na wataalamu na kupelekwa kwa wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao ambayo yamefanyiwa kazi na kujumuishwa kabla ya kupitishwa na Tume.
Wadau waliotoa maoni yao ni pamoja na Vyama vya Siasa, Taasisi za Dini, Serikali, Taasisi za Umma, Asasi na Taasisi zisizo za Kiserikali, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.
No comments:
Post a Comment