NCHI ZA SADC ZAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MAONO YAKE KATIKA USIMAMIZI WA MISITU YA MIOMBO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 18 April 2024

NCHI ZA SADC ZAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MAONO YAKE KATIKA USIMAMIZI WA MISITU YA MIOMBO



Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community-SADC) zimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake katika usimamizi na uhifadhi wa misitu miombo hasa katika kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kuelekea nishati safi ifikapo mwaka 2030.

Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe.Filipe Jaciton Nyusi akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 18,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika Mkutano wa Kimataifa unaohusu Misitu ya Miombo jijini Washington DC nchini Marekani.


“Kikubwa nchi zimeweza kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akitoa maelekezo mbalimbali kwetu sisi kama Wizara na Sekta katika kuhakikisha kwamba misitu ya miombo inalindwa kwa nguvu kubwa, na kwa namna ambavyo amechukua uamuzi thabiti wa kuhakikisha kwamba inapofika mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80 ya wananchi watakuwa wameachana na matumizi wa kuni na mkaa na watakuwa wamejielekeza katika nishati safi ya kupikia” Mhe. Kairuki amesisitiza.


Amesema kuwa misitu ya miombo nchini Tanzania na katika ukanda wa kusini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa misitu ambao unasababishwa na ukataji wa miti usiozingatia sheria, taratibu na kanuni, moto, kilimo cha kuhamahama, uharibifu wa vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabia nchi.


Aidha, amefafanua kuwa kupitia mkutano huo, wadau mbalimbali wameanza kuonesha nia ya kusaidia mpango wa utekelezaji wa Azimio la Maputo la mwaka 2022 kuhusu ulinzi na uendelezaji wa misitu ya miombo.


Amesema lengo la Mkutano huo ni kuona namna ya kuendeleza Azimio la Maputo katika kulinda na kuendeleza Misitu ya Miombo ambapo takribani asilimia 93 ya misitu ya Tanzania ni miombo ambayo pamoja na mambo mengine, inatunza wanyamapori , vyanzo vya maji na huduma nyingine za kijamii.


Naye, Kamishna Uhifadhi wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa kupitia mkutano huo nchi za SADC zimekuwa na majadiliano kuhusu kutafuta namna ya kushirikiana baina ya nchi hizo na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kupata rasilimali fedha na kukuza ujuzi na utaalamu kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa misitu hiyo.


Ameongeza kuwa kongamano hilo limehitimishwa na hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi ambapo amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kushirikiana katika kubadilishana taarifa , kukabiliana na masuala ya uharibifu wa mifumo ya ikolojia ya miombo hususan biashara haramu za mazao ya misitu na wanyamapori katika ukanda wa SADC.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Deusdedith Bwoyo amesema kuwa mkutano huo umekuwa ni wa kipekee na muhimu ambapo nchi 11 zimebaini kuwa umoja ni nguvu na kwamba kila nchi haiwezi kusimamia kwa ufanisi mkubwa misitu yake na hivyo, zimekutana na kujadili kwa pamoja changamoto za misitu ya miombo na namna ya kuunganisha nguvu na kutafuta rasilimali fedha katika usimamizi na uendelezaji wake kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (kulia) akiwa na baadhi ya Mawaziri wa nchi za SADC katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024.
Rais wa Jamhuri ya Watu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jaciton Nyusi (katikati) akifuatilia mawasilisho kuhusu misitu ya miombo kutoka kwa wawakilishi wa nchi za SADC katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo jijini Washington DC nchini Marekani leo Aprili 18,2024. Kushoto kwake ni Waziri wa Ardhi na Mazingira wa Msumbiji, Mhe.Ivete Maibaze na Balozi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani, Mhe. Hilda Suka-Mafdze (kulia).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso