WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Timu ya Mawaziri itakwenda Wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani kuungana na timu ya watalaamu ili kufanya tathmini ya pamoja kutokana na athari zilizosababishwa na mafuriko yaliyotokea wilayani humo.
Ametoa kauli hiyo usiku wa kuamkia leo katika hafla ya Futari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma.
“Sisi ndio tunaratibu Idara ya Maafa kitaifa, hapa tunapozungumza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama pamoja na Katibu Mkuu, Dk Jim Yonaz wako njiani wanaelekea mkoani Pwani, mto rufiji umejaa na kata nne zipo kwenye maji, Mawaziri wengine wa Sekta ikiwemo Afya, Kilimo, Mifugo nao pia wanakwenda ili kuimarisha uratibu wa zoezi,” amesema kiongozi huyo.
Viongozi wengine walioshiriki katika iftar hiyo ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mary Maganga na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment