JESHI LA MAGEREZA MWANZA LAJIPANGA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 29 April 2024

JESHI LA MAGEREZA MWANZA LAJIPANGA KUJITOSHELEZA KWA CHAKULA


Jeshi la Magereza mkoa wa Mwanza limedhamiria kufanya mapinduzi zaidi katika uzalishaji wa aina mbalimbali, hasa kilimo, ili kuongeza usalama wa chakula kwa jeshi lenyewe na jamii inayolizunguka.

Mkuu wa Magereza Mkoa (RPO) Kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Justin M. Kaziulaya aliyasema hayo juzi wakati wa kikao cha kujadili ushirikiano baina ya ofisi ya kilimo ya Mkoa na Jeshi la Magereza kilichofanyika ofisini kwake, akafafanua kwamba:.


Miongoni mwa jamii itakayonufaika na ziada ya chakula ni taasisi za hospitali na shule, hatua ambayo pia itasaidia kuimarisha lishe za walengwa.


“Sambamba na uzalishaji, tunaendelea pia na majukumu yetu ya msingi kama vile urekebishaji wa tabia za wafungwa, na muhimu zaidi kuhakikisha askari wote wanaendelea kutii kanuni na taratibu za miongozo ya Jeshi pamoja na maagizo na maelekezo ya viongozi mbalimbali.


“Tunapokea maelekezo kuanzia Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka pamoja na viongozi wengine. Sitakuwa tayari kuona askari au mtumishi yeyote akienda kinyume.


Alisistiza utayari wa Jeshi la Magereza kujikita zaidi katika uzalishaji, huku akitoa shukrani zake kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambayo imekua ikishirikiana na jeshi hilo kutoa wataalam na elimu juu ya jinsi gani nguvu kazi ya wafungwa inaweza kuleta tija katika uzalishaji uliokusudiwa.


Vile vile ushirikiano huo unahakikisha wafungwa wanapatiwa nyenzo za kuzalisha, kusimamia na kuratibu shughuli za uzalishaji kupitia kilimo, ufugaji, pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.


“Tunawashukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambayo baadhi ya wataalamu wake wa kilimo mmeweza kufika hapa leo kuangalia maendeleo ya shughuli za kilimo, ikiwemo bustani za mbogamboga.


“Ujio wenu wa mara kwa mara una manufaa lukuki kwetu, lakini zaidi kutoa ujuzi kwa wafungwa wetu ambao wataendelea kuutumia katika jamii hata baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao, hatimaye kujitegemea kiuchumi na kuacha kabisa uharifu".


Aliitaka jamii kutambua kwamba zama za sasa sio za askari magereza kuadhibu wahalifu kwa namna yoyote ile, bali kushirikiana nao katika nyanja mbalimbali, hasa urekebishaji tabia ili wawe raia wema wakati wote.


Alisistiza kwamba ushirikiano kati ya askari na wafungwa ni mkubwa, ikiwa ni hatua ya kulifanya Jeshi la Magereza kuzidi kuaminika katika jamii kwamba ndicho chombo pekee cha urekebishaji tabia kwa wafungwa, na si chanzo cha kusababisha kifo au ulemavu kwa wanaotimikia kifungo.


Mtaalamu wa kilimo kutoka ofisi ya Mkoa, Innocent Keya, alisema mipango ya kupita kila magereza iliyopo Mwanza ni endelevu, sio tu kuwapatia wafungwa mbinu za ukulima bora, bali hata kutafuta fursa za masoko kwa njia mbalimbali , ikiwemo maonyesho ya nanenane ambayo hufanyika kila mwaka.


Jeshi la Magereza kupitia Mkoa wa Mwanza ina vituo vyake vitano vya Magereza ambavyo ni pamoja na Gereza Kuu Butimba, Gereza Kasungamile, Gereza Ukerewe, Gereza Ngudu pamoja na Gereza Magu huku katika Magereza hayo yakijishughulisha na shughuli mbalimbali kama vile kilimo cha Mpunga, Mahindi, ufugaji, bustani za mboga kwa ajili ya biashara na wafungwa, pia kwa kutumia kiwanda cha uzalishaji bidhaa mbalimbali za ngozi kilichopo gereza kuu Butimba.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso