Mgodi wa Uchimbaji madini ya dhahabu wa Bucreef uliopo mkoani Geita umeingia makubaliano na Shirika la madini la Taifa (Stamico), kuchoronga mita 10,000 za miamba ili kuongeza thamani na uhai wa mgodi kwa miaka mingi zaidi.
Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba wa kuchoronga miamba hiyo wenye thamani ya Sh5.01 bilioni, Meneja Mkuu wa kampuni ya Buckreef Gaston Mujwahuzi amesema kwa sasa mgodi huo una uhai wa miaka 17 mbele.
Mgodi huo unaomilikiwa kwa ubia wa Serikali na kampuni ya TRC Gold Tanzania pia umesaini mkataba wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, wenye thamani ya Sh420 milioni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwase amesema kusainiwa kwa mkataba huo kunatokana na shirika kujibadilisha na kujiendesha kibiashara.
Amesema kandarasi ya uchorongaji miamba waliyoipata itawawezesha kufanya tafiti zaidi ili kuongeza thamani na maisha ya mgodi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema uwepo wa mgodi wa Buckreef umeongeza shughuli za uwekezaji kwenye kata ya Rwamgasa na kufungua masoko kwa wajasiriamali wadogo.
Kutokana na hali hiyo Shigela amewataka wananchi kutumia vizuri fursa hizo ili kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.
No comments:
Post a Comment