Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Maendeleo Ufaransa (AFD) ambao umeongozwa na Naibu Mtendaji Mkuu, Marie-Hélène Loison.
Mazungumzo hayo yamejikita katika uwekezaji na utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya maji na usafi wa mazingira Ziwa Victoria katika Jiji la Mwanza na Aweso ameeleza umuhimu wa upanuzi wa mradi huo unaokwenda kumaliza uhaba wa maji katika jiji la Mwanza. Uongozi wa AFD umeridhia jambo hilo.
Ikumbukwe, awamu ya kwanza ya mradi huo imetekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.
Kwa upande mradi uliopo mkoani Morogoro, Aweso amewasilisha ombi la nyongeza ya uwekezaji wa fedha zitakazowezesha kuongeza ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji pamoja na miundombinu ya ujenzi wa majitaka ambapo SFD walitenga Euro milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya majisafi pekee.
Aidha, Wizara ya Maji imewasilisha ombi la fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kutoa maji Ziwa Tanganyika kuyepeleka mikoa ya Katavi na Rukwa.
Naibu Mtendaji Mkuu wa AFD amesema kombi hilo limepokelewa na litafanyiwa kazi na kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa.
Aweso amesema hatua hiyo ni mafanikio ya ajenda iliobebwa na Wizara ya Maji katika ziara ya kikazi nchini Ufaransa na itachangia kufanikisha upatikanaji wa maji katika maeneo ambayo miradi ya ujenzi wa miundombinu imekamilika na inaendelea.
No comments:
Post a Comment