Umoja wa vikundi mbalimbali vilivyopo kituo cha mabasi cha CDT wamemuomba mkuu wa Wilaya ya Kahama Mheshimiwa Mboni Mhita kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika eneo hilo ikiwemo urejeshwaji wa fedha zinazodaiwa kuliwa na baadhi ya viongozi waliotoka madarakani.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita akisikiliza kero za wananchi mbalimbali wanaofanya shughuli zao katika kituo cha mabasi cha CDT mjini Kahama akiwa sambamba na kaimu mkurugenzi Manispaa ya Kahama, Clemence Mkusya
NA NEEMA NKUMBI-KAHAMA
Hayo yamesomwa katika risala yao iliyosomwa na Shukuru Peter, mbele ya mkuu wa wilaya, Mboni Mhita March 20, 2024 kwenye mkutano ulioandaliwa na wananchi mbalimbali wanaofanya shughuli katika eneo hilo.
Katika risala hiyo wamebainisha changamoto kuwa baadhi ya viongozi waliotoka madarakani wa kituo hicho cha mabasi yaendayo maeneo tofauti katika Wilaya ya Kahama na nje ya Kahama kuwa viongozi hao walijibinafsisha fedha kiasi cha shilingi milioni 19.8 ambazo ni fedha za umoja wa vikundi zilizopatikana kutokana na ada za uanachama, ulinzi na faini.
Pia wananchi hao wameomba kuwezeshwa mikopo ya gharama nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi sambamba na hilo wameomba kituo hicho kufungwa taa ili waweze kufanya kazi usiku na mchana.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita amewaahidi kutatua changamoto hizo na kumtaka kamanda wa jeshi la Polisi Wilaya ya Kahama (OCD) kuwafuatilia waliochukua fedha ili waweze kurudisha na ametoa wiki moja waitwe wasema watalipa hizo fedha kwa namna gani.
Aidha DC Mboni Mhita amewataka akina mama kufanya kazi kwa bidii kuliko kusubiri kuletewa kwani fursa ziko nyingi mfano katika sekta ya madini kuna wawekezaji wengi wanaohitaji kuwekeza hivyo watumie fursa hiyo kuuza vitu mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi.
No comments:
Post a Comment