WAKALA wa Barabara nchini(Tanroads)mkoa wa Ruvuma,imewatoa hofu watumiaji wa barabara kuu ya Songea-Mangaka kwamba daraja la mto Muhuwesi wilayani Tunduru ambalo lilipata athari ya moja ya sehemu yake kusogea pembeni kwa sasa liko salama.
Na Mwandishi wetu-Tunduru
Hayo yamesemwa jana na meneja wa Tanroads mkoani hapa Mhandisi Saleh Juma, baada ya kukagua kazi ya marekebisho ya daraja hilo linalounganisha mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani ya Lindi,Mtwara Pwani na Dar es slaam.
Alisema,Tanroads kwa kumtumia mkandarasi imefanya kazi ya kurudisha sehemu ya kipande kilichotoka sehemu yake na hata maji yalivyopita juu kwa mara ya pili hayakuathiri miundombinu ya daraja hilo muhimu kwa uchumi wa mikoa ya kusini na nchi kwa ujumla.
Salehe alisema,iwapo itatokea tena daraja hilo kufunikwa na maji watumiaji watalazimika kusubiri hadi yatakapopungua kwa ajili ya usalama wao ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Aidha alieleza kuwa,wamemtafuta mhandisi mshauri ambaye atashauri namna bora ya kuboresha daraja hilo ili liendane na kiwango cha maji kinachopita katika mto Muhuwesi kama daraja hilo lipandishwe juu au lijengwe lingine.
Msimamizi wa kitengo cha matengenezo Tanroads mkoa wa Ruvuma mhandisi Roman Mbukwini alisema,kwa sasa kazi inayofanyika ni kuimarisha baadhi ya sehemu ya barabara ambazo zimeathirika na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi wilayani humo.
Alisema,mvua hizo zimesababisha baadhi ya maeneo ya barabara maji kupita chini ya ardhi na kuharibu miundombinu,lakini tayari serikali kupitia Tanroads inafanya marekebisho ili kurahisisha shughuli ya usafiri na usafirishaji.
Mkazi wa Tunduru Daniel Peter,ameshauri daraja hilo lipandishwe juu na mto Muhuwesi upanuliwe ili maji yasipite juu ya daraja kwa usalama wa wananchi na miundombinu ya daraja.
No comments:
Post a Comment