Dar es Salaam. Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori amewakemea baadhi ya Makandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea kuacha tabia hiyo huku akieleza Bodi haitasita kuwafutia usajili wa kampuni zao.
Alisema kwa sasa Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa miradi mingi kutekelezwa na Makandarasi wazawa lakini kuna baadhi wamekuwa wakitumia fursa hiyo kuijengea taswira mbaya tasnia hiyo kwa kufanya kazi bila kuzingatia weledi.
Hayo aliyasema leo Dar es Salaam wakati akiongea na Makandarasi zaidi ya 170 waliokuwa wakishiriki mafunzo ya siku tatu yaliyokuwa yanalenga kuwajengea uwezo na ujuzi wa namna ya kuandaa zabuni, kujaza mikataba, utekelezaji wa mikataba ya ujenzi, elimu ya kodi na namna ya kuzisimamia na kuboresha kazi zao.
“Kwa Makandarasi ambao wataonekana kuichafua tasnia hii kwa kufanya kazi kwa mazoea tunaomba ushirikiano wenu tuweze kuwaondoa kwenye usajili wabakie wale wenye sifa zinazotakiwa na si vinginevyo,”
”Matukio ya ovyo yanapotokea yanachafua tasnia na yanawaharibia nyie wote,wako Makandarasi wengi wazuri lakini kuendelea kuwapuuza wanaofanya matukio ya ovyo hawatatujengea heshima, tunaomba ushirikiano mkiwaona basi wanafanya hivyo msikae kimya,” alisema Nkori.
No comments:
Post a Comment