Serikali imeahidi kutoa kipaumbele kwenye suala la changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa madini nchini, ili kuiwezesha sekta hiyo kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipokutana na wafanyabiashara wa madini wa soko la madini la Kahama, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na hatimaye kuzitafutia ufumbuzi.
"Mtakumbuka niliwahi kufika hapa Kahama kwa changamoto ya utoroshaji, lakini niliwaahidi kuwa nitatenga siku maalumu ili nije niwasikilize changamoto zenu na kwa pamoja tushauriane namna bora ya kuzitatua kwa masilahi mapana ya nchi yetu na sekta ya madini kwa ujumla."
" Rais Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo mahususi ya kusimamia sekta ya madini kikamilifu na kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili wachimbaji na wafanyabiashara ya madini tunazitatua,"amesisitiza Mavunde.
Waziri Mavunde amebainisha kuwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha inafuatilia kwa ukaribu na kusimamia sekta ya madini ili kubaini iwapo changamoto zilizopo ni za kiusimamizi au mfumo.
Amesema lengo ni kuona kama zinasababishwa na sheria zetu Serikali ifuate taratibu za kupeleka bungeni mapendekezo ya kubadili sheria kuinua zaidi biashara ya madini nchini.
No comments:
Post a Comment