RC MNDEME AONGOZA MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI SHINYANGA, ATAJA VIPAUMBELE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 8 March 2024

RC MNDEME AONGOZA MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI SHINYANGA, ATAJA VIPAUMBELE

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewaongoza wanawake katika Maadhimisho ya Siku Ya Wanawake Duniani Mkoa wa Shinyanga ambapo ametumia fursa hiyo kuwasihi wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi zijazo huku akiwakumbusha kujihadhari na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwani kwa mkoa huo bado hali si shwari.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Mkoa wa Shinyanga yakiongozwana kauli mbiu ‘Wekeza kwa Wanawake ; Kuharakisha Maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii’ yamefanyika leo Ijumaa Machi 8,2024 katika viwanja vya Sabasaba Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na makundi mbalimbali ya wanawake.


Amesema kutokana na tafiti ya kisayansi iliyofanyika mwaka 2022 (THIS 2022), mkoa wa Shinyanga una ushamiri wa maambukizi ya VVU ya asilimia 5.6 ambayo ipo juu ya kiwango cha taifa cha asilimia 4.5.


“Serikali ya mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuratibu udhibiti wa maambukizi ya VVU kwa kutoa huduma mbalimbali za tiba na matunzo. Pamoja na jitihada zote zinazofanyika za kuwawezesha wanawake, nawakumbusha kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU kwani hupelekea kupunguza nguvu kazi, kuongezeka kwa yatima, wajane na hatimaye kusababisha jamii kuzama kwenye wimbi la umaskini”,amesema Mhe. Mndeme.


Mkuu huyo wa mkoa pia amewakumbusha kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kufuata maelekezo ya watalaam wa afya na kuhakikisha usafi wa mazingira katika maeneo yanayowazunguka.


Amesema serikali imeendelea na jitihada za kuwezesha wanawake kiuchumi ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi mbalimbali za kifedha.


“Mkoa wa Shinyanga unaungana na nchi zingine duniani kuratibu na kusimamia uwekezaji katika kundi la wanawake kwa kuweka vipaumbele katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wanawake, kuendeleza jitihada za serikali na wadau wa maendeleo za kupinga mila na desturi zenye madhara zinazopelekea kukosekana kwa usawa kijamii, kiuchumi na kisiasa”,amesema Mhe. Mndeme.


Amesema pia Mkoa wa Shinyanga unaendelea kuboresha na kusimamia utoaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma na kusimamia chanjo mbalimbali ikiwemo chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi inayotolewa kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka 14.


“Tunaendelea kuboresha mazingira ya elimu kwa kuhakikisha mkoa unakuwa na shule bora za wasichana, kuhamasisha matumizi ya teknolojia rahisi kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali ili kuongeza ubora wa bidhaa wanazotengeneza zikiwemo batiki, sabuni, mafuta, viungo vya chakula n.k”,amesema.


“Kipaumbele kingine ni kusimamia programu Jumuishi ya taifa ya malezi na makuzi na maendeleo ya watoto kuanzia miaka 0 hadi 8 na kuendelea kuratibu na kusimamia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, mfuko wa wanawake na kupitia kwa wadau mbalimbali walio ndani na nje ya mkoa”,ameongeza Mhe. Mndeme.


Mhe. Mndeme amewashukuru wadau mbalimbali waliotoa michango yao kufanikisha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri, Idara ya maendeleo ya jamiiTANROADS, Shirika la YAWE, Life Water International, Rafiki SDO, TCRS, ADD international na ICS.


Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoa wa Shinyanga Dkt. Regina Malimi ambaye ni katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Taifa amesema miongoni mwa changamoto zinazowakwamisha wanawake ni mikopo umiza hivyo kuwataka wanawake kuacha kujiingiza kwenye mikopo hiyo.


Kwa upande wao, Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga akiwemo Mhe. Santiel Kirumba, Dkt. Christina Mzava na Lucy Mayenga na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi wamewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika malezi ya watoto pamoja na kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utaofanyika mwaka huu.


Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amekabidhi misaada mbalimbali iliyotolewa na wadau wa maendeleo ikiwemo chakula kwa ajili ya watoto wanaolelewa katika shule AGAPE na mifuko 31 ya saruji kwa ajili ya ujenzi Bweni katika shule ya Buhangija iliyotolewa na Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Shinyanga (TPF- NET Mkoa wa Shinyanga).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso