RC MNDEME AAGIZA KILA ENEO LENYE MKUSANYIKO WA WATU KUWEKWA MAJI TIRIRIKA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday 7 March 2024

RC MNDEME AAGIZA KILA ENEO LENYE MKUSANYIKO WA WATU KUWEKWA MAJI TIRIRIKA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme akizungumza wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) leo Alhamisi Machi 7,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Shinyanga (Shycom).


                Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewaagiza Maafisa Afya mkoani Shinyanga kuhakikisha sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu kuwe na maji tiririka ya kunawa mikono na kuchukua hatua za kisheria pale watakapojiridhisha kuna mtu kwa maksudi hataki kufuata kanuni za afya na hivyo kusababisha ugonjwa wa kipindupindu kuendelea kusambaa.


Mhe. Mndeme ametoa agizo hilo leo Alhamisi Machi 7,2024 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Walimu Shinyanga (Shycom) kikilenga kujadili mambo mbalimbali kuhusu Mkoa wa Shinyanga.


Mhe. Mndeme ugonjwa wa kipindupindu bado upo ndani ya Mkoa wa Shinyanga katika baadhi ya halmashauri ambapo mpaka sasa kati ya wagonjwa 216 walioripotiwa, wagonjwa 127 wamekutwa na vimelea vya kipindupindu hivyo kuagiza hatua madhubuti zichukuliwe ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa kipindupindu.


"Halmashauri mbili zimeweza kuudhibiti ugonjwa wa kipindupindu ambazo ni Manispaa ya Kahama (siku 29 hawana mgonjwa) na Halmashauri ya Kishapu (siku 9 hawana mgonjwa). Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeendelea kupata wagonjwa kipindupindu baada ya kukaa kwa muda wa siku 13 bila wagonjwa (Februari 12- 25,2024. Na kwa Manispaa ya Shinyanga kata za Ndala na Kambarage zimeathirika zaidi",amesema Mhe. Mndeme.


Mkuu huyo wa Mkoa amesema pia bado mkoa wa Shinyanga unakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya sukari hivyo amewaelekeza Mawakala wote wanaouza sukari ndani ya mkoa wa Shinyanga waendelee kuzingatia maelekezo ya serikali kwa kuuza sukari kwa bei elekezi ambapo bei ya rejareja ni kati ya shilingi 2,800/= hadi 3,000/= kwa kilo moja na kwa bei ya jumla ni kati ya shilingi 2,650/= hadi 2,800/= ambapo kwa mfuko wa kilo 50 ni kati ya shilingi 132,500/= na shilingi 140,000/=.


Mhe. Mndeme pia ameziagiza Halmashauri kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji ambayo hayataathiri shughuli za kilimo na utunzaji maliasili ili kuongeza uzalishaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo kutokana na kwamba Shinyanga kuna Machinjio ya kisasa huku akiwataka maafisa mifugo kutembelea wafugaji na kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa hali ambayo italeta mazingira rafiki kwa wafugaji waache kuhama mkoa kwenye kutafuta malisho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso