MHESHIMIWA RAIS SAMIA ANATAKA WATANZANIA WATOKE KWENYE UMASKINI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 27 March 2024

MHESHIMIWA RAIS SAMIA ANATAKA WATANZANIA WATOKE KWENYE UMASKINI


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua Kiwanda cha kuwekea mifumo ya kupasha na kutunza joto katika mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).


Akizindua mradi huo katika Kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora, Dkt. Biteko amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP umefikia asilimia 27 ikiwa ni kielelezo cha usimamizi madhubuti wa Rais wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambao wamekuwa vinara katika kuhakikisha mradi unafanyika kwa wakati na viwango vya kimataifa.

Amesema utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri ikiwemo suala la utwaaji wa ardhi ambapo malipo yamefanyika kwa asilimia 99.2, ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhi mafuta Chongoleani Tanga umeshaanza na kufikia asilimia 32 na gati ya kupakia mafuta katika eneo la Chongoloeani umefikia asilimia 36.

Vilevile ametoa pongezi kwa Serikali ya Uganda kwa kuiona Tanzania kama mdau muhimu kwenye maedeleo ya nchi yao na kwamba Serikali ya Tanzania inatambua mchango huo na kuuthamini.

Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ya Tanzania na Uganda zipo kwenye majadiliano ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa Bomba la Gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda ikiwa ni maelekezo ya viongozi Wakuu wa Nchi hivyo Wizara ya Nishati itayasimamia kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Rais Samia anataka kuwaletea maendeleo Watanzania wote, kuwatoa kwenye umaskini na kuwainua kiuchumi kwa kushirikiana na Sekta binafsi hivyo ni muhimu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Sekta binafsi na kutowakwamisha.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso