NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameagiza kuweka Mpango Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika vituo ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa.
Dk Biteko ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi nchini Tanzania tarehe 25 Machi, 2024 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.
Dk Biteko amewataka kujadili kwa kina namna bora ya kubuni mbinu zitakazowezesha kuongeza kasi ya kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya hasa zile zenye upungufu mkubwa.
Pia, ameagiza kuainisha mikakati ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelimishwe kuhusu njia za kuzuia magonjwa, umuhimu wa chanjo na njia zingine za kudumisha afya bora.
Dk Biteko amesisitiza kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo ya kuboresha.
No comments:
Post a Comment